Dar es Salaam
Makumbusho ya Taifa yamepata heshima kubwa baada ya mgeni maalum – Mke wa Rais wa Finland – kutembelea eneo hilo na kushuhudia kwa macho vivutio vya kitamaduni na historia ya Tanzania. Ziara hiyo imefungua ukurasa mpya wa mashirikiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Finland, hasa katika sekta ya misitu na utalii wa kihistoria.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, alisema uhusiano wa Tanzania na Finland umekuwa wa kihistoria na wenye mafanikio, ukijikita zaidi kwenye misitu, tafiti na teknolojia ya uhifadhi.
“Finland ni nchi inayotegemea misitu kwa uchumi wake. Tumekuwa tukishirikiana kwa zaidi ya miaka 40. Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliwahi kutembelea nchi hiyo mwaka 1973 – ishara ya uhusiano wa muda mrefu,” alifafanua Dkt. Abbas.
Mke wa Rais wa Finland hakuja peke yake – Rais wake anatarajiwa kutembelea makumbusho hayo kesho, ikiwa ni sehemu ya ziara yao rasmi nchini Tanzania. Katika ziara hiyo, Tanzania itanufaika na mradi mkubwa wa dola za Kimarekani milioni 20 (takribani Shilingi bilioni 40), utakaowezesha kukuza sekta ya misitu kwa kutumia maarifa na teknolojia kutoka Finland.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga, alisema ujio wa mgeni huyo ni zaidi ya heshima – ni fursa ya kuonyesha kuwa utalii wa makumbusho nao unakua na una mchango mkubwa kwenye uchumi.
“Zamani tulizoea kuona watalii wakielekea mbuga za wanyama tu, lakini sasa makumbusho yameanza kuvutia wageni wa kimataifa. Hii ni hatua kubwa ya awamu ya sita katika kuibua vyanzo vipya vya utalii,” alisema Dkt. Lwoga.
Ameongeza kuwa Makumbusho ya Taifa yanapanga kushirikiana na Finland kwenye tafiti, uhifadhi wa mali kale kwa teknolojia ya kisasa, pamoja na kubadilishana wataalamu wa utamaduni na historia.
“Kama taifa, tunapaswa kuthamini urithi wetu. Ziara hizi si tu ishara ya mahusiano mazuri bali ni mwaliko kwa Watanzania kwenda makumbusho, kujifunza kuhusu historia yao na kuenzi utamaduni wao,” alisema.
Ziara hii ya kifalme imeacha alama – si tu kwenye ubao wa kumbukumbu wa Makumbusho ya Taifa – bali pia kwenye mioyo ya Watanzania na marafiki wa maendeleo kutoka Finland
0 Comments