Na mwandishi wetu
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa kwamba baadhi ya wanasiasa katika wilaya ya Ngorongoro wamekuwa wakifanya ushawishi kwa njia ya fedha ili kuwazuia wananchi wanaotaka kuhama kwa hiyari wasihame kutoka ndani ya hifadhi.
Baadhi ya wanasiasa hao na wanaharakati wamekuwa wakitafuta fedha hizo kupitia baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani na nje ya nchi ili waendelee kufanya ushawishi kwa wananchi na hatimaye waendelee kubaki ndani ya hifadhi kwa maslahi yao binafsi.
Inaonesha wazi kuwa kinachofanywa na wanasiasa hao kina lengo la kutaka kutetea nafasi zao za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao ambao baadhi ya wanaofanya hivyo wanaamini kuwa ikiwa wananchi watahama katika tarafa ya Ngorongoro na wao watapoteza vyeo vyao kwa kukosa kura.
Lakini kwa mtu aliyefika ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na kuona maisha halisi ya wananchi hao atakubali ukweli uliopo kwamba kuendelea kuishi kwa watu katika hifadhi hiyo ni kuhatarisha ustawi wa hifadhi lakini na maendeleo ya jamii hiyo hasa kubaki maskini na hivyo serikali kuwajibika kuwahudumia wanananchi hao.
Ukifika katika hifadhi ya Ngorongoro utastaajabu wananchi wakiishi katika maisha duni huku Watoto wadogo wakikosa haki yao ya msingi ya kupata elimu badala yake kutumika kufanya shughuli za uchungaji wa mifugo wakati wanasiasa wengi wa eneo hilo wakiishi nje ya hifadhi huku watoto wao wakipata elimu bora.
Wananchi hao wamekuwa wakiishi katika mazingira ambayo hayawaruhusu kufanya shughuli nyingine yoyote ya kimaendeleo zaidi ya uchungaji ambapo inaarifiwa kuwa hata wanyama wengi wanaowafuga ni wa hao wanasiasa.
Ni jukumu la baadhi ya wanasiasa na wanaharqkati wa Ngorongoro kubadilika kwani kuendelea kutumia nafasi zao kwa maslahi yao ni kuhatarisha ustawi wa wananchi walio wengi ambao nao bila kujua wamekuwa wakiwasikiliza.
Wito kwa serikali ni kutorudi nyuma katika utekelezaji wa zoezi kuelimisha, kuandikisha na kuwahanisha hilo na kuongeza nguvu katika kuwahamisha wananchi walioko tayari kuhamia maeneo ambayo yametengwa au kule wananchi walipochagua kuhamia.

0 Comments