CHATANDA AZIPONGEZA HALMASHAURI ZA MBEYA KUTOA MIKOPO YA ASILIMIA 10 KWA WALENGWA HALISI

 










Mwenyekiti wa UWT Taifa, Ndg. Mary Pius Chatanda (MCC), amezipongeza Halmashauri za Mkoa wa Mbeya kwa kusimamia utoaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri na kuhakikisha inawafikia walengwa halisi.

Chatanda ameyasema hayo Agosti 7, 2026, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Songwe na Mbeya, ambapo alitembelea na kujionea vikundi vya wanawake vinavyonufaika na mikopo hiyo pamoja na mafunzo na mitaji ya biashara.

Amesema miradi hiyo imekuwa na mchango katika kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi na kuongeza kipato cha familia.

Aidha, Chatanda amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii na Madiwani wa Viti Maalum kushuka katika kata, matawi na vijiji ili kutoa elimu, kuunda vikundi na kuwasaidia wanawake wenye uhitaji, badala ya kusubiri changamoto zifike ofisini.

“Tusiwe madiwani wa kukutana na changamoto kwenye ofisi pekee; twendeni tukawatumikie wanawake waliotuchagua, tuwasikilize, na tuwape ushauri utakaowatoa kwenye changamoto zao,” alisisitiza Chatanda.

Vilevile, amezipongeza UWT Mkoa wa Mbeya, wabunge na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao uliowezesha ujenzi wa nyumba za watumishi na kuanza kwa ujenzi wa majengo ya UWT katika kila wilaya mkoani humo.

Akizungumzia masuala ya kisiasa, Chatanda amewakumbusha wanachama wa CCM na makundi mbalimbali kuanza kujiandaa mapema kwa ajili ya Uchaguzi wa Chama unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.

Ziara hiyo inaratibiwa na Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UWT Taifa na inahusisha mikoa 12 ya Tanzania Bara, ikiwa na lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025/2030 pamoja na uhai wa Chama na Jumuiya zake.

Post a Comment

0 Comments