TEMEKE, 1 Agosti 2026
Akiendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Jimbo la Temeke, Mbunge wa Jimbo la Temeke, Mh. Mariam Nassoro Kisangi, ametembelea maeneo mbalimbali ya Kata ya Temeke.
Katika ziara hiyo, Mh. Kisangi alimtembelea mmoja wa wajasiriamali walionufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Alipata fursa ya kujionea maendeleo ya biashara hiyo na kusisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya mikopo hiyo ili kuongeza kipato, kukuza biashara na kuchangia maendeleo ya familia na jamii.
Aidha, Mh. Kisangi alikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara katika kata hiyo na kusikiliza maoni pamoja na changamoto zinazowakabili wananchi. Miongoni mwa kero zilizojitokeza ni athari zinazotokana na malori makubwa kupita katika maeneo ya makazi, jambo linaloharibu miundombinu ya barabara na kuhatarisha usalama wa wananchi. Aliahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto hizo.
Katika kuimarisha mawasiliano na wananchi, Mh. Kisangi pia alikutana na wazee na vijana katika kijiwe cha jamii, ambapo alisikiliza maoni yao, kupokea mapendekezo mbalimbali na kuwahimiza kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Kata ya Temeke.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu wa Mbunge wa Jimbo la Temeke wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza wananchi ana kwa ana na kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo.


0 Comments