Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Taasisi ya CYPG imewakutanisha wadau mbalimbali katika Kongamano la National Development and Innovation Dialogue 2026 lililofanyika leo katika eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujadili nafasi ya ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa CYPG, Shedrak E. Zadock, alisema maendeleo endelevu ya Tanzania yanahitaji ushirikiano wa wadau kutoka sekta ya umma, sekta binafsi, taasisi za elimu, asasi za kiraia na vijana wenye mawazo ya kibunifu.
Alisema kongamano hilo limetoa jukwaa la kubadilishana uzoefu, kujadili fursa zilizopo na kuibua suluhisho bunifu zitakazochangia ukuaji wa uchumi, maendeleo ya jamii na kuongeza ushindani wa Tanzania katika nyanja mbalimbali.
"Ubunifu ni nguzo muhimu ya maendeleo. Tunahitaji kuendelea kuwawezesha vijana na wadau wengine ili wawe sehemu ya kutengeneza suluhisho za changamoto zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla," alisema Zadock.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi wa taasisi mbalimbali, wataalamu, wajasiriamali, wanafunzi na wadau wa maendeleo, ambao walijadili masuala ya ubunifu, teknolojia, uongozi na ushirikiano kama nyenzo za kuharakisha maendeleo endelevu nchini.
0 Comments