QUEEN SENDIGA AONGOZA JITIHADA ZA KUSAIDIA WATOTO NJITI KUPITIA MANYARA TANZANITE MARATHON

 

MANYARA

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amesema uwepo wa idadi kubwa ya watoto njiti mkoani humo ndio sababu kuu ya kuanzishwa kwa mbio za hisani za Manyara Tanzanite Marathon, zinazolenga kusaidia huduma kwa watoto hao.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mhe. Sendiga amesema mbio hizo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono huduma zinazotolewa na Serikali kwa watoto njiti na kuongeza ushiriki wa jamii katika kusaidia mahitaji yao.

"Uwepo wa watoto njiti mkoani Manyara ndio chanzo cha kuanzisha mbio hizi za hisani za Manyara Tanzanite Marathon. Na hii ndio sababu ya kuongozana na Mganga Mkuu wa mkoa wetu wa Manyara ambaye yeye anaweza kutuelezea vizuri kitaalamu," amesema.

Amesema mkoa huo una idadi kubwa ya watoto njiti na ongezeko lao limekuwa likiongezeka, jambo lililosababisha kuhitajika kwa mpango maalum wa kuwasaidia zaidi.

"Tuna watoto wengi njiti na ongezeko lao ni kubwa sana. Mbali na juhudi zinazofanywa na Serikali, tuliona kwamba tuna kila sababu ya kuja na mpango mzuri wa kuweza kuwasaidia zaidi hawa watoto," amesema Mhe. Sendiga.

Mbio za Manyara Tanzanite Marathon zinatarajiwa kufanyika tarehe 22 Agosti, 2026 mkoani Manyara, zikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kushiriki katika kusaidia huduma za afya na ustawi wa watoto njiti.

Post a Comment

0 Comments