Tanzania Yataka Wafanyabiashara Wake Kuchangamkia Masoko ya Nje

 








Dar es Salaam, Oktoba 22, 2025 — Serikali imehimiza wafanyabiashara wa Kitanzania kuchangamkia fursa za biashara nje ya nchi kupitia Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), huku ikiahidi kushirikiana nao kuimarisha Diplomasia ya Uchumi.


Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, wakati wa kufungua Mkutano Mkuu Maalum wa TCCIA Taifa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Thabiti Kombo, alisema kuwa masoko ya kimataifa yamefunguka na Tanzania inapaswa kuyaingia kwa nguvu.


Alitoa mfano wa soko la China, ambalo linahitaji tani bilioni moja za zao la soya, huku Tanzania ikizalisha tani 36 pekee, akisisitiza kuwa hiyo ni nafasi ya dhahabu kwa Watanzania kuongeza uzalishaji.


> “Soko la soya tayari lipo China na ni beauty free — hakuna ushuru wa kuingia. Wakulima na wafanyabiashara wanatakiwa wachangamkie hii fursa,” alisema Waziri Kombo.




Waziri huyo alisema wafanyabiashara wa Kitanzania tayari wameanza kufungua biashara moja kwa moja katika nchi nyingine kupitia Chemba, na akawatia moyo wengine kuiga mfano huo kwa mazao mbalimbali, akitaja kahawa kama zao linalouzwa kwa dola moja kwa kilo katika soko la dunia.


Katika hatua nyingine, Waziri Kombo alieleza kuwa Tanzania ina uwakilishi katika nchi 50, lakini shughuli za kibiashara zimekuwa zikifanyika kati ya nchi 6 hadi 10 pekee, hivyo kuna haja ya kupanua juhudi hizo.


> “Tumeahidi kuwa kila Balozi atakuwa na jukumu la kuwasaidia wafanyabiashara moja kwa moja. Nimemuelekeza Balozi Ulanga kushughulikia hilo. Pia, tumeomba kuandaliwa mkataba rasmi wa Diplomasia ya Uchumi kati ya Chemba na Wizara,” aliongeza.




Amesema serikali itaendelea kushirikiana na Chemba katika maeneo ya teknolojia, mifumo ya taarifa na mafunzo kwa wanachama wake, ikiwa ni sehemu ya kuijenga sekta binafsi kwa nguvu zaidi.


> “Katika database yenu hakikisheni mnawaweka wanachama kwa makundi: walioko kwenye kilimo na walioko kwenye biashara. Hii itatusaidia kupanga mikakati kwa ufanisi zaidi,” alisisitiza.




Waziri pia alitaka uwakilishi wa Chemba uimarishwe zaidi kwa kushirikisha vijana, watu wenye ulemavu na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora), akibainisha kuwa makundi hayo ni muhimu katika ajenda ya maendeleo ya taifa.


Mwisho, aliwataka viongozi wa Chemba kuhakikisha kuwa mpango wao wa maendeleo wa miaka mitano unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo tayari imezinduliwa rasmi.

Post a Comment

0 Comments