MH RIDHIWANI KIKWETE AENDELEA NA KAZI JIMBONI AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO NA KUWAPA WANANCHI MREJESHO.





Mbunge wa Jimbo la Chalinze na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete wiki hii yupo Jimboni akifanya ziara ya kikazi katika Kata ya Kibindu ambapo kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo.


Julai 23, 2026 Mhe. Kikwete alianza ziara kwa kukagua Shule mpya ya Msingi Chapuku iliyojengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu kupitia Mradi wa BOOST. Shule hiyo imeanzishwa kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Kibindu ambayo hapo awali ilikuwa na zaidi ya wanafunzi 2,000, hali iliyokuwa ikiathiri mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Akipokea taarifa, alifurahishwa na utekelezaji wa mradi huo akisema umeondoa changamoto ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa eneo hilo.


Akiendelea na ziara yake, Mheshimiwa Kikwete alikagua ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi cha Kibindu kinachoendelea kujengwa. Mradi huo ulianzishwa na kundi la WhatsApp la “Kibindu Tunayoitaka” na kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wananchi wa vijiji vyote vya Kata ya Kibindu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Ndugu Abubakar Mlawa, Ofisi ya Mbunge pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kupitia mapato ya ndani.

Jumla ya Shilingi za Kitanzania 42,450,000 zimekusanywa kupitia michango hiyo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho. Mheshimiwa Kikwete aliwapongeza wananchi na wadau wote waliojitokeza kuchangia, akisema ushirikiano huo unaonesha uzalendo, mshikamano na dhamira ya pamoja ya kuimarisha usalama na kudumisha amani katika Kata ya Kibindu na Jimbo la Chalinze kwa ujumla.


Kikwete alisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika miradi ya maendeleo ni nguzo muhimu inayochochea maendeleo endelevu na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ubora unaostahili.

Akihitimisha ziara yake, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete alitembelea Kituo cha Afya Kibindu ambapo alikagua miundombinu iliyopo, kuzungumza na watumishi wa afya pamoja na kuwasalimia wagonjwa waliokuwa wakipatiwa huduma. Katika ziara hiyo, alibaini baadhi ya mahitaji ya miundombinu ambayo bado yanahitaji kuboreshwa ili kituo hicho kikidhi kikamilifu miongozo ya utoaji wa huduma za afya.


Mheshimiwa Kikwete aliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha miundombinu inayokosekana inajengwa na iliyopo inaboreshwa, huku akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta za elimu, afya na usalama. Alisema maendeleo yanayoonekana katika Kata ya Kibindu ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Serikali, viongozi na wananchi, na kwamba ushirikiano huo unapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Post a Comment

0 Comments