Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, tarehe 29 Aprili 2026 amezindua rasmi awamu ya pili ya mpango wa kupokea mawazo bunifu kutoka kwa umma, unaolenga kupanua wigo wa kodi na kuboresha huduma za ukusanyaji mapato nchini.
Uzinduzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Johari Rotana jijini Dar es Salaam, ambapo Mwenda alisema mpango huo ni sehemu ya juhudi za kuishirikisha jamii moja kwa moja katika kuboresha mifumo ya kodi na kuongeza mapato ya serikali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenda aliwashukuru Watanzania walioshiriki katika awamu ya kwanza, akibainisha kuwa jumla ya washiriki 5,681 walijitokeza kutoa mawazo yao kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, jambo linaloonesha imani kubwa ya wananchi kwa taasisi hiyo.
Alieleza kuwa kati ya mawazo yote yaliyowasilishwa, 106 yaliingia katika hatua ya tathmini, huku washindi tisa wakitangazwa na mawazo yao kuanza kufanyiwa kazi. Alisisitiza kuwa hata mawazo ambayo hayakushinda hayakupotea, bali yanaendelea kutumika kuboresha mifumo ya kiutawala na utekelezaji wa kodi bila kuhitaji mabadiliko ya sheria.
Mwenda alisema TRA imejifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza na kufanya maboresho makubwa katika awamu ya pili, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfumo utakaomwezesha mshiriki kufuatilia hatua zote za wazo lake kuanzia kupokelewa, tathmini hadi uamuzi wa mwisho.
“Tunataka wananchi wawe na imani kuwa mawazo yao yanathaminiwa na yanapitia mchakato wa haki na uwazi. Ndiyo maana tumeweka mfumo utakaotoa mrejesho katika kila hatua,” alisema Mwenda.
Katika kuimarisha zaidi uwazi, alisema TRA haitahusika moja kwa moja katika mchakato wa kuchagua washindi, bali jukumu hilo litatekelezwa na timu huru ya wataalamu wenye weledi na uadilifu ili kuhakikisha haki inatendeka.
Aidha, Mwenda alibainisha kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuishirikisha jamii katika usimamizi wa kodi, akisisitiza kuwa mapato yanayokusanywa ni kwa manufaa ya taifa. Aliongeza kuwa ushirikishwaji wa wananchi utasaidia kupata mawazo yanayoendana na mabadiliko ya kiuchumi, hasa katika zama za biashara za kidijitali.
Alisema mifumo ya biashara imebadilika kwa kasi, huku baadhi ya wafanyabiashara wakifanya shughuli zao mtandaoni, hali inayohitaji mbinu mpya za usimamizi wa kodi ili kuhakikisha usawa na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
Kuhusu motisha, Mwenda alisema washindi wa awamu ya kwanza walipatiwa zawadi kama ilivyoahidiwa, ambapo mshindi wa kwanza alipokea shilingi milioni 50, wa pili milioni 30, na wengine hadi milioni 20. Aliongeza kuwa zawadi hizo zimeboreshwa zaidi katika awamu ya pili ili kuvutia ushiriki mpana zaidi.
Mwenda alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika awamu hiyo ya pili, akisisitiza kuwa kila wazo lina thamani katika maendeleo ya taifa.
“Kwa kushiriki, si tu unaisaidia TRA, bali unaisaidia nchi yako. Utakuwa sehemu ya historia ya maboresho ya mfumo wa kodi nchini,” alisisitiza.
Awamu ya pili ya mpango huo inatarajiwa kuibua mawazo mapya yatakayosaidia kuongeza mapato ya serikali sambamba na kurahisisha mazingira ya biashara kwa wananchi na wawekezaji nchini.



0 Comments