ADDIS ABABA, 27 APRILI 2026
Na Mwandishi Wetu
Makamu wa zamani wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn Boshe, ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kubadili kabisa mfumo wa matumizi ya rasilimali zake za madini, akisisitiza kuwa ni wakati wa bara hilo kuacha kuwa msambazaji wa malighafi na badala yake kujenga viwanda vya kijani vinavyoongeza thamani ya rasilimali hizo ndani ya Afrika.
Akizungumza katika Jukwaa la Kikanda la “Harnessing Africa’s Critical Minerals for Green Industrialisation” lililofanyika katika makao makuu ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kiuchumi kwa Afrika (UNECA), Addis Ababa, Hailemariam alisema dunia ipo katika kipindi cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayoongozwa na hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi na mwelekeo wa matumizi ya nishati safi.
Alisema katika mabadiliko hayo, mahitaji ya madini muhimu kama cobalt, lithium, copper, manganese na rare earths yameongezeka kwa kasi kutokana na matumizi yake katika utengenezaji wa betri, magari ya umeme na mifumo ya nishati mbadala, hivyo Afrika ina nafasi kubwa ya kunufaika zaidi endapo itajenga viwanda vyake vya ndani.
Hata hivyo, alibainisha kuwa licha ya Afrika kumiliki sehemu kubwa ya rasilimali hizo, bado wananchi wake wanakabiliwa na umaskini kutokana na kuendelea kusafirisha malighafi bila kuongeza thamani, hali aliyoitaja kuwa ni lazima ibadilike haraka.
Hailemariam alisisitiza kuwa Afrika inapaswa kuhamia katika hatua ya juu ya mnyororo wa thamani kwa kuanzisha viwanda vya kusafisha na kuchakata madini, viwanda vya betri, pamoja na sekta za chuma na alumini ya kijani, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira, kukuza uchumi na kuimarisha ushindani wa bara hilo kimataifa.
Pia alisema mafanikio ya viwanda hivyo yanategemea uwepo wa miundombinu imara na nishati ya uhakika, akihimiza uwekezaji katika nishati jadidifu kama jua, upepo na jotoardhi ili kuendesha viwanda kwa gharama nafuu na kwa uendelevu wa mazingira. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya usafirishaji kama reli, barabara na maeneo maalum ya kiuchumi (SEZs).
Akizungumzia ushirikiano wa kikanda, Hailemariam alisema Soko Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ni nyenzo muhimu ya kuunganisha nchi za Afrika katika mnyororo mmoja wa uzalishaji, akibainisha kuwa hakuna nchi moja inayoweza kujenga kikamilifu sekta ya betri au magari ya umeme peke yake bila kushirikiana na nyingine.
Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, nchi moja inaweza kuchimba madini, nyingine ikayachakata, na nyingine ikatengeneza bidhaa za mwisho, hali itakayoongeza nguvu ya kiuchumi ya Afrika katika soko la dunia.
Hata hivyo, alionya kuhusu changamoto zinazoikumba sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na ukwepaji kodi, mikataba isiyo na uwiano, pamoja na athari za mazingira na jamii, akitoa wito wa kuimarishwa kwa taasisi za usimamizi ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na manufaa kwa wananchi.
Kwa upande wa wawekezaji na washirika wa maendeleo, Hailemariam alisema Afrika inahitaji ushirikiano wa haki unaolenga uwekezaji wa viwanda, uhamishaji wa teknolojia na kuhakikisha bara hilo linakuwa sehemu ya kweli ya mnyororo wa thamani wa uchumi wa kijani duniani.
Akihitimisha hotuba yake, alisema mustakabali wa Afrika hauwezi kujengwa juu ya uuzaji wa malighafi pekee, bali kupitia viwanda, ujuzi na matumizi ya busara ya rasilimali zake kwa manufaa ya wananchi wake wote.
“Ni wakati wa Afrika kutumia rasilimali zake kujenga uchumi wa viwanda unaoweka msingi wa ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema.


0 Comments