Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama leo april 30,2016 Mkoa wa Tabora, imefanikiwa kuteketeza ekari 68 za mashamba ya bangi na kukamata gunia 133 za dawa hiyo katika operesheni maalum iliyofanyika katika hifadhi za misitu ya Igombe River wilayani Uyui na Nyahua wilayani Sikonge mkoani Tabora.
Katika operesheni hiyo, watu saba (7) wamekamatwa wakihusishwa na kilimo na usambazaji wa bangi katika maeneo hayo ya hifadhi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 30, 2026 katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mamlaka hiyo inaendesha operesheni maalum ya kuteketeza dawa za kulevya zinazozalishwa nchini.
“Sasa hivi tuko kwenye kampeni maalum kuhakikisha tunateketeza dawa za kulevya zinazozalishwa nchini, hasa baada ya kupungua kwa dawa za kulevya za viwandani,” alisema Lyimo.
Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiwezesha mamlaka hiyo kuanzisha ofisi ya DCEA Kanda ya Magharibi yenye makao yake mkoani Tabora, hatua aliyosema imeongeza ufanisi na kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Lyimo pia aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha kufanikisha operesheni hiyo, akibainisha kuwa bangi nyingi zimekuwa zikipandwa katika maeneo ya mapori na hifadhi ili kujificha.
“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hatutakubali uhalifu huu uendelee. Tutahakikisha tunafanya operesheni endelevu katika maeneo yote na kuchukua hatua kali kwa wanaojihusisha na kilimo na uzalishaji wa dawa za kulevya,” alisisitiza Lyimo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Paul Chacha, ameipongeza DCEA kwa kazi kubwa ya kudhibiti dawa za kulevya mkoani humo, na kuwaagiza askari wa TFS kuweka kambi katika maeneo ya misitu na hifadhi ili kukomesha kabisa kilimo cha bangi katika mkoa huo.
.jpg)
.jpg)
.jpg)



0 Comments