Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa wito kwa wataalamu wa ndani kuchangamkia fursa zinazotokana na miradi mikubwa ya ujenzi nchini.
Akizungumza Wakati akimuwakilisha Naibu waziri mkuu na waziri Wa Nishati na Madini Doto Biteko katika Kongamano la Tano la Bodi ya Usajili wa Wakadiriaji Majenzi na Wahandisi jijini Dar es Salaam Oktoba 29, 2024, Mpogolo amesema ni muhimu kwa wataalamu wa ndani kutumia uwezo wao katika miradi ya serikali ili kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje.
Mpogolo amebainisha kuwa, ingawa wataalamu wa ndani wanakabiliwa na changamoto ya mitaji midogo, wanapaswa kuongeza juhudi zao kushiriki katika miradi hiyo badala ya kuruhusu serikali kutumia wataalamu wa nje, hali inayosababisha upotevu wa fedha za kigeni. Amehimiza wataalamu wa ndani kushirikiana kwa kuondoa ubaguzi katika utoaji wa fursa za kazi ili kufanikisha miradi hiyo kwa umoja.
Aidha, Mpogolo amekemea tabia ya baadhi ya wataalamu wa ndani kuwatafuta wataalamu wa nje na kushirikiana nao huku wao wakipata sehemu ndogo ya faida. Alisisitiza kuwa mshikamano na ushirikiano wa kitaifa ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya sekta ya ujenzi na kuimarisha uchumi wa nchi.
Kongamano hilo lililenga kujadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya ujenzi, pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali.

0 Comments