Dar es Salaam, Oktoba 1 – Mjasiriamali kijana na mlezi wa vipaji, Chichi Mayeye, ameongoza uzinduzi wa mashindano ya hotuba yajulikanayo kama Speech Competition katika viwanja vya Kinzudi, Goba, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kujieleza, kujiamini, na kuwaandaa kuwa viongozi bora wa baadaye.
Mashindano hayo ambayo ni ya aina yake yamehusisha shule sita za sekondari kutoka maeneo ya Goba na vitongoji vyake, zikiwemo Goba Sekondari, Fahar Sekondari, Kinzudi, na Matosa Sekondari. Katika hatua ya awali, mshindi mmoja alipatikana, huku wengine wakionesha uwezo mkubwa wa kujieleza kwa umakini na ushawishi wa hali ya juu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Chichi Mayeye alieleza kufurahishwa na mwitikio wa wanafunzi, akisema kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa harakati kubwa za kuibua na kukuza vipaji vya vijana kote nchini.
“Nimefurahi sana kwa jinsi vijana walivyojitokeza na walivyojitahidi. Tumeanza hapa Dar es Salaam, lakini ndoto yangu ni kuona mashindano haya yakifikia kila kona ya Tanzania, na hatimaye dunia nzima,” alisema Mayeye.
Zaidi ya kutoa jukwaa kwa vijana kuonesha uwezo wao wa kujieleza, Mayeye alisema kuwa washindi wawili wa mashindano hayo watapatiwa zawadi ya fedha taslimu pamoja na nafasi ya kipekee ya kusafiri hadi Marekani kwa ziara ya mafunzo na kukuza ujuzi.
“Nimeamua kufanya hivi kwa sababu naamini huu ni uwekezaji mkubwa kwa kizazi kijacho. Tunahitaji viongozi wenye ujasiri, uwezo wa kufikiri kwa kina (critical thinking), na uwezo wa kujieleza kwa ufasaha. Speech Competition itakuwa chachu ya mabadiliko hayo,” aliongeza.
Mayeye alisisitiza kuwa huu ni mwanzo wa safari ndefu ya kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya mawasiliano, uongozi, na maadili. Aliwataka wadau wa elimu, wazazi na serikali kushirikiana katika kuunga mkono jitihada hizo ili kuhakikisha kuwa vijana wa Tanzania wanapata fursa sawa ya kujiendeleza.
“Maono yangu ni makubwa. Natarajia kuona mashindano haya yakikua na kufikia ngazi ya kitaifa na kimataifa. Dunia inapaswa kujua kuwa Tanzania ina vijana wenye uwezo mkubwa, na tunapaswa kuwasaidia kuangaza,” alisema.
Watazamaji waliohudhuria hafla hiyo walieleza kuvutiwa na ubunifu wa wanafunzi na walitoa pongezi kwa Chichi Mayeye kwa moyo wake wa kizalendo na kujitoa kwake katika kuimarisha mustakabali wa vijana wa taifa.
Mashindano haya yanatarajiwa kuendelea katika mikoa mingine nchini, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa kuwajengea vijana uwezo wa kuongoza na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao.





0 Comments