JNHPP KUZINDULIWA RASMI AGOSTI 22


Serikali inatarajia kuzindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) kilichopo Rufiji, mkoani Pwani, Agosti 22, 2026.

Uzinduzi huo utafanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema mradi huo umegharimu takribani Sh trilioni 7.452 na kwa sasa unazalisha MW 2,115 kati ya MW 4,648 za uwezo wa jumla wa uzalishaji wa umeme nchini.

Amesema hadi Mei 31, 2026, JNHPP ilikuwa imechangia takribani asilimia 44.9 ya umeme ulioingia katika gridi ya Taifa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, hivyo kuwa chanzo muhimu cha umeme nchini na kusaidia kupunguza changamoto za upungufu wa umeme.

Wakati wa ujenzi, mradi huo ulitoa ajira kwa takribani wafanyakazi 12,000, ambapo asilimia 99 walikuwa Watanzania. Bwawa la mradi lina uwezo wa kuhifadhi takribani mita za ujazo bilioni 33 za maji, likiwa na manufaa pia katika kilimo cha umwagiliaji, utalii na shughuli nyingine za kiuchumi.

Serikali imesema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa nishati na kuchochea uzalishaji, uwekezaji na ukuaji wa uchumi nchini.

Post a Comment

0 Comments