JOHNSON SARAKIKYA ASEMA KWAMBA UTEUZI WA NDEJEMBI NI IMANI KWA VIJANA

 



Arusha — Aliyekuwa mtia nia wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki mwaka 2025, Johnson Sarakikya, amesema hatua ya Halmashauri Kuu ya CCM kumpendekeza Waziri wa Nishati, Deogratius John Ndejembi, kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania ni ishara ya kuendelea kuaminiwa kwa vijana katika nafasi za uongozi nchini.

Sarakikya ametoa kauli hiyo leo Agosti 27, 2026, kupitia ukurasa wake wa Instagram, akimpongeza Ndejembi kwa kuaminiwa na Halmashauri Kuu ya CCM inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema hatua hiyo inaonyesha kuwa vijana wanaendelea kupewa nafasi kutokana na uwezo, uchapakazi na uwajibikaji wao katika utekelezaji wa majukumu ya kitaifa.

Sarakikya amesema uteuzi huo unapaswa kuwa hamasa kwa vijana wengine kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kujenga uwezo na kuwa tayari kutumikia Taifa wanapopewa dhamana.

Aidha, amesema kuaminiwa kwa Ndejembi katika nafasi hiyo ni ujumbe kwa vijana kwamba bado wana nafasi kubwa ya kushiriki katika uongozi na maendeleo ya Taifa.

Sarakikya amempongeza Ndejembi na kumuombea kwa Mungu ampe hekima, busara na uwezo wa kutekeleza majukumu yake mapya, hususan katika kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan.

“Ndejembi, tunakuombea kwa Mungu akutunze na kukuongoza katika majukumu ya kumsaidia Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Uteuzi huu unatupa imani sana sisi vijana,” amesema Sarakikya.

Amesema vijana wanapaswa kutumia fursa kama hiyo kujifunza, kuongeza uwezo na kuendelea kujenga mazingira ya kuaminiwa katika majukumu mbalimbali ya uongozi na utumishi wa Taifa.

Post a Comment

0 Comments