RUBY INTERNATIONAL LIMITED YATUNUKIWA TUZO KWA KUTANGAZA VITO VYA TANZANIA KATIKA SOKO LA KIMATAIFA

 


Kampuni ya Ruby International Limited imetunukiwa tuzo ya Outstanding Contribution to the Global Promotion of Tanzanian Gemstones, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kutangaza na kuitangaza Tanzania kupitia madini ya vito katika soko la kimataifa. 

Tuzo hiyo imetolewa katika Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026), uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Tuzo hiyo imekuja kufuatia ushiriki wa kampuni hiyo katika maonesho mbalimbali ya kimataifa ya madini na vito, yakiwemo maonesho ya Bangkok Gems and Jewellery Fair nchini Thailand pamoja na Hong Kong Jewellery and Gem Fair. 

Kupitia maonesho hayo, Ruby International Limited imekuwa sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye utajiri mkubwa wa madini ya vito, huku ikifungua fursa za kibiashara na kujenga mahusiano na wadau wa sekta hiyo kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, mkoani Morogoro, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Ruby International Limited, Salim Hasham, ameeleza kufurahishwa na kutambuliwa kwa mchango wa kampuni hiyo, akisema tuzo hiyo ni chachu ya kuongeza juhudi katika kuitangaza sekta ya madini ya vito ya Tanzania kimataifa.

"Kutunukiwa tuzo hii ni heshima kubwa kwetu na ni uthibitisho wa juhudi tunazozifanya katika kuitangaza Tanzania kupitia madini yake ya vito. Tunapata hamasa zaidi ya kuendelea kushiriki katika majukwaa ya kimataifa ili kuhakikisha vito vya Tanzania vinapata nafasi na kutambulika katika masoko ya Dunia," amesema Hasham.

Aidha, Hasham amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini, hususan katika utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani na biashara ya madini ya vito. 

Amehimiza uwekezaji katika maeneo hayo unaweza kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira, kuingiza fedha za kigeni na kuinua kipato cha wananchi. 

Ameongeza kuwa Ruby International Limited itaendelea kushiriki katika juhudi za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia utajiri wake wa madini ya vito.

Post a Comment

0 Comments