Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mawakala wa Meli Tanzania, Abel Uronu, amesema kuwa rasilimali watu wenye ujuzi na utaalamu katika sekta ya bandari ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Uronu ameyasema hayo wakati akizungumza na wahitimu wa Chuo cha Bandari, ambao wamemkaribisha kuzungumzia mchango wa sekta ya bandari katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050, akieleza kuwa ni muhimu kutathmini hatua ambazo sekta hiyo imepiga kutoka ilipoanza hadi ilipofikia sasa, pamoja na matarajio ya maendeleo ya baadaye.
Amesema ili kufikia malengo ya dira hiyo, sekta ya bandari inahitaji kutoa huduma bora na zenye ufanisi katika bandari, vituo vya kupokelea na kuhifadhi mizigo ya ndani (ICD), pamoja na maeneo mengine yanayohusiana na shughuli za kibandari.
Amesema iwapo sekta hiyo itawekeza katika elimu, ujuzi, teknolojia na utoaji wa huduma bora, Tanzania itaweza kufikia malengo makubwa yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya 2050.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wahitimu wa Chuo cha Bandari (Alumni), Robert Mellami, amesema wahitimu wa chuo hicho pamoja na wadau wengine wa sekta ya uchukuzi wana jukumu muhimu la kutafakari namna wanavyoweza kutumia taaluma na uzoefu wao kuchangia maendeleo ya taifa.
Mellami amesema maendeleo ya sekta ya bandari hayapaswi kupimwa kwa kuangalia miundombinu pekee, bali pia uwepo wa wataalamu wenye ujuzi, maarifa na uwezo wa kusimamia shughuli mbalimbali za sekta hiyo.
Ameeleza kuwa rasilimali watu ni sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya uchukuzi na bandari, kwani hata miundombinu ya kisasa inahitaji wataalamu wenye uwezo wa kuitumia na kuhakikisha inatoa matokeo yanayotarajiwa.
Aidha, amebainisha kuwa kwa sasa Chuo cha Bandari ni chuo pekee nchini Tanzania kinachotoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya bahari, hivyo kina nafasi muhimu katika kuandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya sekta hiyo na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050.

.jpg)

0 Comments