Na: Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Naibu spika wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ilala,Azan Zungu amewataka vijana kufanya kazi kwa kuwekeza kwenye mambo yenye tija ikiwemo kilimo bila kuangalia elimu zao.
Zungu ameyasema hayo alipokuwa akifungua kongamano la vijana kazini lililoandaliwa na taasisi ya Amo Foundation kusheherekea siku ya vijana duniani sambamba na kutoa mafunzo kwa vijana juu ya fursa zilizopo katika nyanja mbalimbali ili waweze kujikimu ambapo kongamano hilo limefanyika katika hoteli ya Hollyday in jijini Dar es salaam.
Aidha amesema kama vijana watajiepusha na makundi na kufanya kazi kwa bidii bila kujali elimu walizonazo hali hiyo itawapelekea kujiinua kiuchimi,huku akiwataka kutojiingiza katika mashirika yanayokwenda kinyume na maadili ya kitanzania pamoja na kuacha zinaa ili wafanikiwe.
''njia ya kwanza ya ufukara ni zinaa kwani inawafanya vijana wengi wasifanye kazi na waache kuhudumia familia zao kisa zinaa,nawasihi achaneni na mambo ya zinaa mpige kazi na nyie wasichana kama mvulana amekupenda mwambie akajitambulishe kwenu na akuoe''alisema Zungu.
Kwa upande wake mkurugenzi wa taasisi ya Amo Foundation Bi Amina Goodsay amesema taasisi yake imeamua kufanya kongamano hilo la kijana kazini ili kusheherekea siku ya vijana duniani na kuwafundisha namna wanaweza kujikimu maishani kwa kujishughulisha.
Amesema taasisi hiyo itatoa vifaa mbalimbali vya biashara kwa vijana na kuwasimamia katika kufanya kazi zao ikiwemo bodaboda,cherehani,majiko ya mama lishe pamoja na vifaa vya saluni kwa vijana hao.
Bi Amina ameongeza kuwa taasisi ya Amo Foundation itaendelea kuwaunga mkono vijana nchini kwa kuwawezesha kiuchumi na kuwapa mafunzo ya jinsi ya kufanya biashara zao.
Naye Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogoro amesema dhana ya uwajibikaji ni kubwa sana kwa vijana hivyo wanapaswa kuwajibika.
''vijana wanatamani za juu kuliko kufanya kazi kwenye nafasi walizopo na matokeo yake wanapunguza uwajibikaji hivyo niwasihi vijana wawe wawajibikaji''alisema DC Mpogoro

0 Comments