TPSF YATOA MAFUNZO YENYE LENGO KUIMARISHA UTUNZAJI WA MALIASILI

 

Meneja Mradi wa Kuhifadhi Maliasili kwa ufadhili wa USAID Godfrey Mondi akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

Afisa Wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Dolorosa Maricky akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.




Na Mwandishi Wetu. 

IMEELEZWA kuwa Taasisi za kifedha kama benki pamoja na Taasisi za Mawasiliano ni wadau muhimu katika kuhakikisha tunafanikiwa kutunza Maliasili dhidi ya ujangili.

Hayo yamebainishwa leo Desemba 7, 2023 jijini Dar es Salaam na Afisa Wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Dolorosa Maricky akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa warsha iliyoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kwa ushirikiano na TAWA yenye lengo la kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Sekta ya Benki pamoja na Mawasiliano ili kuweza kushirikiana kwa pamoja kudhibiti Maliasili.

Maricky amesema kwamba kwa sasa vitendo vya ujangili vimepungua na kwamba Serikali inashirikiana vyema na sekta binafsi kuhakikisha hali ya ujangili isiendelee kujitokeza pamoja na kulinda Maliasili.

“Lazima kuwepo na ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi, hivyo warsha kama hizi zinasaidia kuleta umoja kati ya serikali na Sekta binafsi katika kuhakikisha tunapambana na ujangili, ,hivyo tunaendelea kutoa mafunzo kwa wadau wenzetu ili tushirikiane pamoja katika kuhifadhi Maliasili hizi,” amesema Maricky.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Kuhifadhi Maliasili kwa ufadhili wa USAID Godfrey Mondi amesema kuwa mradi wa kuhifadhi Maliasili unatekelezwa kwa muda wa miaka mitano.

Amesema kuwa kumekuwepo na biashara haramu ya Wanyamapori, hivyo sasa ni wakati wa taasisi za serikali na sekta binafsi kushirikiana kwa pamoja ili kuwezesha kutunza rasilimari zilizopo kwa ajili ya vizazi vilivyopo navijavyo.

“Leo TPSF tumeshirikiana na TAWA kufanya semina hii kwa washiriki wa sekta ya benki na taasisi za Mawasiliano kwani hawa ni wadau muhimu ambao tunashirikiana nao katika kupambana na hali ya ujangili,mradi huu wa kuhifadhi Maliasiri unafanyika kwa muda wa miaka mitano na umefadhiliwa na wenzetu wa USAID,” amesema Mondi. 

Post a Comment

0 Comments