MBUNGE WA WATU WENYE ULEMAVU AANZA ZIARA YA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WALIO NA ULEMAVU KATIKA NGAZI YA MTAA – KILIMANI, MANZESE

 





Na Mwandishi Wetu

Mbunge wa Watu Wenye Ulemavu ameanza rasmi juhudi za kushughulikia changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu kwa kushuka moja kwa moja hadi ngazi ya mtaa, ambapo leo tarehe 6january 2025 alitembelea Mtaa wa Kilimani uliopo Manzese kufuatia taarifa ya uwepo wa mgonjwa mwenye ulemavu anayehitaji msaada wa haraka.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mbunge huyo alisema kuwa licha ya kuwa ni Mheshimiwa na kiongozi wa ngazi ya kitaifa, ameona umuhimu wa kuanza utatuzi wa changamoto za wananchi kuanzia maeneo wanayoishi, badala ya kusubiri taarifa kupitia ngazi za juu pekee.


“Changamoto za watu wenye ulemavu zipo karibu sana nasi. Hata kama mimi ni Mheshimiwa, nikaona ni muhimu nianze kwenye mtaa wako, nishuke chini nione hali halisi ya wananchi wangu,” alisema Mbunge huyo.


Alieleza kuwa alipokea taarifa hiyo siku ya Jumapili kupitia simu kutoka Zanzibar, ikieleza kuwa katika eneo hilo kuna mgonjwa mwenye ulemavu anayeishi katika mazingira magumu na anayehitaji msaada wa haraka.


“Nilipopigiwa simu nikaona nisikae mbali. Nikaamua kuja mwenyewe ili nitambue changamoto iliyopo, niweze kuona namna bora ya kushirikiana na viongozi wa eneo hili kumpatia msaada unaohitajika,” aliongeza.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa kama mwakilishi wa watu wenye ulemavu, ana wajibu wa kimaadili na kisheria kuhakikisha kundi hilo linapata haki zao za msingi ikiwemo huduma za afya, dawa za mahitaji maalum, pamoja na ulinzi wa kijamii.

Aidha, aliweka wazi nia yake ya kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mitaa kupitia Mwenyekiti wa Mtaa na viongozi wengine wa msingi ili kubuni na kutekeleza mikakati ya kudumu ya kuwahudumia watu wenye ulemavu.

“Tunatamani tufanye kazi kwa ushirikiano na Serikali yako, Mwenyekiti. Ushirikiano huu utatusaidia kuwafikia walemavu wengi zaidi na kutatua changamoto zao kwa ufanisi,” alisema Mbunge huyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilimani, Manzese, Hamisi Omary Ngoma, alimpongeza na kumshukuru Mbunge huyo kwa kuchukua hatua ya vitendo ya kushuka hadi mtaani pamoja na timu yake, akieleza kuwa hatua hiyo imewapa matumaini makubwa wakazi wa eneo hilo.

“Ninashukuru sana leo kupata ugeni wa Mheshimiwa Mbunge wa Watu Wenye Ulemavu pamoja na timu yake, wamefika mtaani kwetu kuangalia kwa macho changamoto zinazowakabili walemavu wetu,” alisema Mwenyekiti Ngoma.

Alibainisha kuwa Mtaa wa Kilimani ni miongoni mwa mitaa ya kwanza kuanza rasmi kuibua changamoto za watu wenye ulemavu, akisema bado kuna vikwazo vingi vinavyohitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali na jamii.

Mwenyekiti huyo alieleza kwa masikitiko kuwa bado kuna baadhi ya wazazi na walezi wanaendelea kuwaficha watoto wenye ulemavu majumbani mwao, hali inayosababisha watoto hao kukosa haki ya msingi ya kupata elimu maalum, huduma za afya na malezi stahiki.

“Changamoto kubwa ni kwamba wapo wazazi wanaowaficha walemavu. Hali hii inatupa wakati mgumu sana sisi viongozi wa mtaa kwa sababu watoto hawa hawapelekwi kwenye vituo vya walemavu wala kupata huduma wanazostahili,” alisema.

Mbali na hilo, Mwenyekiti Ngoma aliiomba Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha dawa na vifaa vya mahitaji maalum kwa watu wenye ulemavu vinapatikana bure au kwa gharama nafuu, ili kupunguza mzigo kwa familia zenye kipato cha chini.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo aliahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Mbunge na timu yake, akisisitiza kuwa uongozi wa mtaa uko tayari kushirikiana kikamilifu katika jitihada za kuwasaidia walemavu.


“Nawaaahidi ushirikiano uliotukuka. Tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa na timu yake, na tutaongozana pamoja kwenda kumuona mgonjwa huyo ili tuone kwa vitendo ni msaada gani unahitajika,” alisisitiza.


Ziara hiyo imepokelewa kwa matumaini makubwa na wakazi wa Mtaa wa Kilimani, huku ikionekana kuwa chachu ya kuimarisha mshikamano kati ya viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo na jamii katika kulinda haki na ustawi wa watu wenye ulemavu.

Post a Comment

0 Comments