AIRTEL AFRICA FOUNDATION YAUNGANISHA SHULE 3,296 NA INTANETI, VIJANA NA WANAWAKE 30,530 WANUFAIKA NA MAFUNZO


Airtel Africa Foundation imesema imeendelea kuleta mabadiliko chanya katika jamii za Afrika kupitia uwekezaji wake katika elimu, ujumuishi wa kidijitali na uwezeshaji wa kiuchumi, ambapo shule 3,296 katika nchi 13 za Afrika ikiwemo Tanzania zimeunganishwa na huduma za intaneti.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka 2025/26 ya taasisi hiyo, zaidi ya dola milioni 6.2 zilitengwa kwa utekelezaji wa miradi chini ya nguzo nne za kimkakati za FEED zinazojumuisha ujumuishi wa kifedha, elimu, utunzaji wa mazingira na ujumuishi wa kidijitali.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kupitia ushirikiano kati ya Airtel Africa Foundation na UNICEF, shule mpya 1,028 ziliunganishwa na intaneti katika mwaka huo, na kufanya jumla ya shule zilizounganishwa kufikia 3,296. Shule hizo zinahudumia wanafunzi zaidi ya milioni mbili na walimu karibu 39,000.

Aidha, zaidi ya wanafunzi milioni 11 wamefikiwa kupitia majukwaa 64 ya kidijitali yanayotoa maudhui ya elimu bila malipo, huku shule saba za umma zikikarabatiwa na nyingine 43 zikiendelea kufanyiwa maboresho kupitia mpango wa Adopt School.

Katika sekta ya elimu ya juu, wanafunzi 257 kutoka Tanzania, Nigeria, Uganda, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walipata ufadhili wa masomo kupitia programu ya Airtel Africa Tech Fellowship inayolenga kukuza taaluma za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).

Vilevile, vijana na wanawake 30,530 walinufaika na mafunzo ya ujuzi wa kidijitali yaliyotolewa kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa.

Mwenyekiti wa Airtel Africa Foundation, Segun Ogunsanya, amesema taasisi hiyo ilianzishwa kwa lengo la kusaidia kuondoa vikwazo vinavyosababisha ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa fursa, hususan katika elimu, teknolojia na maendeleo ya kiuchumi.

Amesema katika mwaka ujao taasisi hiyo inalenga kuunganisha shule nyingine 2,000 na intaneti bila malipo, kuongeza idadi ya shule zinazofaidika kupitia mpango wa Adopt School hadi zaidi ya 80, pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa zaidi ya vijana 600 barani Afrika.

Ogunsanya amesema Airtel Africa Foundation itaendelea kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali ili kuongeza ujuzi, kuimarisha uwezo wa kiuchumi wa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu katika bara la Afrika.

Post a Comment

0 Comments