SERIKALI YAONGEZA NGUVU URUTUBISHAJI WA VYAKULA VIJIJINI


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali imesema imejipanga kuwafikia wakulima wa vijijini wanaotumia mashine za kusagia unga wa mahindi ambazo hazijawekewa vitamini na madini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha lishe na kulinda afya za wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika mkutano wa 40 wa Jukwaa la Wadau wa Urutubishaji Vyakula, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Luitfrid Nnally, alisema serikali imeanza kupeleka mashine maalumu zinazowezesha kuongeza virutubishi kwenye vyakula katika maeneo mbalimbali ya vijijini.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanaotegemea mazao yao wenyewe kwa matumizi ya chakula wanapata virutubishi muhimu vinavyosaidia kuimarisha afya zao.

Nnally alieleza kuwa kupitia mfumo wa usimamizi wa huduma za lishe katika mamlaka za serikali za mitaa, mama lishe wamekuwa wakinunua na kusambaza virutubishi kwa wasindikaji wadogo wa vyakula huku serikali ikiendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni husika.

Aidha, alisema tofauti na miaka ya nyuma ambapo virutubishi vilikuwa vinaagizwa kutoka nje ya nchi, kwa sasa Tanzania ina kiwanda kinachozalisha vitamini na madini ndani ya nchi, hatua ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Urutubishaji Tanzania, Gwao Omar Gwao, alisema wadau kutoka sekta ya umma na binafsi wamekutana kujadili changamoto na fursa zilizopo katika utekelezaji wa mpango wa urutubishaji vyakula nchini.

Alisema urutubishaji wa vyakula kama unga wa mahindi, unga wa ngano, mafuta ya kula na chumvi ni muhimu katika kuzuia matatizo ya kiafya yanayotokana na upungufu wa vitamini na madini mwilini, hususan kwa wanawake wajawazito na watoto.

Gwao alibainisha kuwa mpango huo umeanza kutekelezwa katika mikoa yote 26 ya Tanzania na umefikia zaidi ya wilaya 170, huku lengo likiwa ni kuongeza matumizi ya vyakula vyenye virutubishi kwa wananchi wengi zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA), Walter Miya, alisema taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu kwa wazazi wenye watoto wanaokabiliwa na changamoto za mgongo wazi na vichwa vikubwa.

Alisema utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula unaweza kusaidia kupunguza na hatimaye kutokomeza matatizo hayo katika jamii.

Miya aliongeza kuwa katika ukanda wa Ziwa Victoria pekee, zaidi ya watoto 700 huzaliwa kila mwaka wakiwa na changamoto za mgongo wazi na vichwa vikubwa, hali inayohitaji juhudi za pamoja katika kuimarisha lishe na afya ya jamii.


Post a Comment

0 Comments