AIRTEL AFRICA YAENDELEA KUPUNGUZA PENGO LA KIDIJITALI, YAONGEZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI


Airtel Africa imeendelea kuimarisha juhudi za kupunguza pengo la kidijitali, kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuchochea maendeleo endelevu kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, huduma za kifedha kwa njia ya simu pamoja na matumizi ya nishati safi.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya 2026 iliyotolewa Juni 10, 2026 jijini London, kampuni hiyo inayohudumia nchi 14 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania, imeonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2025/26.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa watu wanaofikiwa na mtandao wa simu wameongezeka hadi asilimia 81.9 kutoka asilimia 81.2 mwaka uliopita, huku upatikanaji wa huduma za mtandao katika maeneo ya vijijini ukiongezeka hadi asilimia 73.1 kutoka asilimia 72.2.

Aidha, matumizi ya simu janja yameongezeka hadi asilimia 49.5 kutoka asilimia 44.8, jambo lililochangia kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za data hadi asilimia 45.9. Programu ya My Airtel pia imeendelea kukua ambapo thamani ya miamala iliyofanyika kupitia mfumo huo imefikia dola za Marekani bilioni 8.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 80 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Katika sekta ya huduma za kifedha, Airtel Money imeongeza idadi ya wateja wake kutoka milioni 44.6 hadi zaidi ya milioni 54, huku thamani ya miamala iliyochakatwa ikifikia takribani dola za Marekani bilioni 196 kutoka dola bilioni 136 mwaka uliopita. Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa asilimia 44.1 ya wateja wa Airtel Money ni wanawake.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema kampuni hiyo itaendelea kupanua huduma za mawasiliano, kifedha na elimu ya kidijitali ili kuwafikia mamilioni ya wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini na yale ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu na huduma hizo.

Alisema pamoja na kuimarisha huduma za mtandao na Airtel Money, kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika matumizi bora ya nishati kwa lengo la kupunguza utegemezi wa dizeli na kuongeza ufanisi wa shughuli zake.

Kwa upande wa elimu na ajira, Airtel Africa iliongeza mtandao wa mawakala wa Airtel Money hadi kufikia milioni 2.4 kutoka milioni 1.7 mwaka uliopita, hatua iliyochangia kuongezeka kwa fursa za ajira na ujasiriamali. Pia, jumla ya shule 3,043 zimeunganishwa na huduma za intaneti bila malipo kupitia ushirikiano wa Airtel Africa Foundation na UNICEF.

Katika juhudi za kulinda mazingira, zaidi ya maeneo 950 ya miundombinu ya kampuni yalihamishwa kutoka matumizi ya nishati isiyounganishwa na gridi ya taifa kwenda kwenye umeme wa gridi ya taifa. Hatua hiyo imechangia kupungua kwa matumizi ya dizeli kwa lita milioni 9.1 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Vilevile, asilimia 94 ya taka zote zilizozalishwa na kampuni zilirejelewa, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 93 mwaka uliopita.

Ripoti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Global Reporting Initiative (GRI) pamoja na miongozo ya sekta ya mawasiliano ya simu ya GSMA, ikionesha dhamira ya Airtel Africa ya kuendelea kuendesha shughuli zake kwa uwajibikaji, uwazi na kuzingatia maendeleo endelevu.

Post a Comment

0 Comments