Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania imeendelea kupanua huduma zake za kidijitali baada ya kuzindua maduka mawili mapya ya kisasa ya kidijitali katika maeneo ya Tunduma na Mwanjelwa mkoani Mbeya, hatua inayolenga kusogeza karibu huduma za mawasiliano na kifedha kwa wananchi na wafanyabiashara.
Uzinduzi huo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa kuboresha huduma kwa wateja na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kidijitali katika maeneo muhimu ya biashara nchini.
Duka la kwanza lilizinduliwa Tunduma, mji unaokua kwa kasi kutokana na shughuli za biashara za mipakani kati ya Tanzania na Zambia pamoja na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika.
Duka hilo lililopo Tunduma Hotel karibu na Benki ya Azania lilizinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Daniel Mwandobo kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Uzoefu kwa Wateja wa Airtel Tanzania, Adriana Lyamba.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Lyamba alisema Tunduma imeendelea kuwa kitovu muhimu cha biashara kutokana na nafasi yake katika usafirishaji na biashara za kikanda.
“Tunduma ni moja ya maeneo muhimu ya biashara yanayounganisha Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Ukuaji wake unatokana na biashara, usafirishaji na shughuli mbalimbali za kiuchumi. Airtel tunaona umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika huduma za mawasiliano, intaneti ya kasi na huduma za kifedha za kidijitali katika eneo hili,” alisema.
Tunduma ni lango muhimu la biashara kati ya Tanzania na Zambia na hutumika kusafirisha mizigo kwenda nchi mbalimbali za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tunduma ina wakazi zaidi ya 219,000 huku idadi hiyo ikiendelea kuongezeka kutokana na ukuaji wa biashara na uwekezaji.
Duka hilo jipya litatoa huduma mbalimbali chini ya paa moja zikiwemo Airtel Money, usajili wa laini, huduma za intaneti, simu janja, huduma kwa wateja pamoja na huduma za kidijitali kwa wafanyabiashara.
Mwandobo alisema uwekezaji huo utasaidia kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi na vijana.
“Biashara za kisasa zinahitaji mawasiliano ya kisasa. Uwekezaji kama huu unasaidia kukuza biashara, kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kutoa fursa kwa vijana wetu,” alisema.
Katika siku hiyo hiyo, Airtel Tanzania pia ilizindua duka jingine la kisasa la kidijitali katika eneo la Mwanjelwa jijini Mbeya, moja ya maeneo makubwa ya biashara katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Duka hilo lililopo Mbasi Fuel Station karibu na duka la Vunja Bei lilizinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon J. Itunda pamoja na Lyamba.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Lyamba alisema Mwanjelwa ni kitovu muhimu cha biashara kwa wakazi wa Mbeya kutokana na shughuli kubwa za biashara zinazofanyika kila siku.
“Mwanjelwa ni moyo wa biashara wa Mbeya. Maelfu ya wananchi hutegemea eneo hili kwa biashara, usafiri na shughuli mbalimbali za kiuchumi. Airtel itaendelea kuwekeza katika huduma za kidijitali na kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi,” alisema.
Eneo la Mwanjelwa lina soko kubwa linalohudumia maelfu ya wafanyabiashara na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Nyanda za Juu Kusini.
Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, Jiji la Mbeya lina wakazi zaidi ya 541,000 na linaendelea kukua kwa kasi kutokana na shughuli za biashara na maendeleo ya mijini.
Airtel Tanzania ilisema uzinduzi wa maduka hayo mawili ni sehemu ya mpango wake wa kuendelea kuimarisha huduma za mawasiliano na kidijitali katika maeneo mbalimbali nchini.

0 Comments