Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Afya, Dkt. Jafar Seif, amesema Serikali imepeleka zaidi ya Shilingi Milioni 235 Bohari ya Dawa (MSD) kwa ajili ya kugharamia vifaa tiba, vitakavyosaidia kukamilika kwa Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mafinga ambayo hupokea wagonjwa takribani 650 kwa siku, wengi wao wakiwa ni waathirika wa ajali za barabarani.
Dkt. Seif, amesema hayo leo, Januari 06, 2026, wakati akikagua miundombinu ya majengo manne (4) yaliyojengwa na Serikali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 3.3, katika hospitali hiyo, ambayo ni ujenzi wa wodi ya wazazi, Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU) pamoja na jengo la kufulia nguo, na sehemu ya kutembelea kutoka jengo moja kwenda jingine (Walkway), hatua inayolenga kuboresha kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za afya katika hospitali hiyo.
“Kwa sasa TAMISEMI tunachoendelea nacho ni kumkumbusha Waziri wa Afya Mheshimiwa Omary Mchengerwa juu ya uhitaji wa vifaa hivyo, ili atusaidie tuvipate mapema na huduma hizi za dharura na za uzazi zianze kutolewa hapa Mafinga kwa ubora ule ule ambao mgonjwa angeupata katika hospitali za rufaa za mikoa au Taifa” amesema Naibu Waziri Dkt. Seif.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Mafinga, Dkt. Victor Msafiri, kukamilika kwa miundombinu hiyo, kunatazamiwa kuboresha utoaji wa huduma za afya, kuongeza uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wengi zaidi, kupunguza rufaa zisizo za lazima na kuokoa maisha ya wananchi, hususani waathirika wa dharura na wagonjwa mahututi.
Hospitali ya Mji Mafinga ni miongoni mwa vituo 30 vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Mji Mafinga, ikihudumia takribani wagonjwa 650 kwa siku, wengi wao wakiwa ni waathirika wa majeraha yatokanayo na ajali za barabarani, kutokana na hospitali hiyo kuwa kando ya Barabara Kuu ya Tanzania –Zambia , hali inayoongeza mahitaji ya huduma za dharura na wagonjwa mahututi.







0 Comments