PDX FESTIVAL KUFANYIKA KIGAMBONI, ZORAVO ATANGAZA USIKU WA MAOMBI NA UIMBAJI WA KIHISTORIA



Dar es Salaam

Tamasha kubwa la Injili linalotarajiwa kuwa la kihistoria, PDX FESTIVAL, linatarajiwa kufanyika Ijumaa ijayo, tarehe 16, katika viwanja vya Mji Mwema, Kigamboni, kuanzia saa moja usiku hadi alfajiri.

Akizungumza na waandishi wa habari, mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili Zoravo amesema wazo la kuandaa tamasha hilo lilitokana na maono aliyoyapata baada ya maombi, akieleza kuwa ni kwa neema na kibali cha Mungu ndipo mpango huo umefanikiwa kutimia.

Zoravo amesema, “Mara nyingi watu wa Kigamboni hulazimika kuvuka kuja upande huu kwa ajili ya matamasha, lakini safari hii sisi tunavuka Ng’ambo kuwafikia wao. Mungu amejibu maombi ya watu wake.”

Ameeleza kuwa PDX Festival itakuwa ni tamasha la usiku mzima (overnight) litakalojikita katika uimbaji wa nyimbo za Injili, maombi ya pamoja na huduma ya uponyaji, akisisitiza kuwa waumini watapata uzoefu wa kipekee wa kiroho.

Katika tamasha hilo, waimbaji wakubwa wa Injili wamethibitisha kushiriki, wakiwemo Rose Muhando, Upendo Nkone, Joel Kavishe, Obby Alpha pamoja na Henric Mruma.

Zoravo ameongeza, “Itakuwa ni experience ya ajabu; tutaimba pamoja na kusali pamoja. Tunaamini Roho wa Mungu anaweza na hakuna kitakachoshindikana.”

Aidha, amewahimiza wananchi wote walioko Dar es Salaam na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi, akiahidi kuwa watakaohudhuria watashuhudia mambo makubwa ya kiimani.

“Kama hujawahi kuona watu wakiimba na watu wakipona kwa pamoja, basi tarehe 16 utashuhudia,” alisisitiza Zoravo.




PDX Festival inatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya Injili kwa mwaka huu, likiwa na lengo la kuimarisha imani, umoja na matumaini kwa waumini na jamii kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments