NANAUKA AZINDUA JUKWAA LA VIJANA,ASEMA ASILIMIA 77.3 YA WATU NCHINI NI VIJANA


 

Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Joel Nanauka, amesema vijana ndio nguzo kuu ya maendeleo ya Taifa kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa nguvu kazi ya nchi, akibainisha kuwa zaidi ya nusu ya nguvu kazi ya Taifa inatokana na vijana.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Youth Platform) uliofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo alikuwa mgeni rasmi, Nanauka alisema takwimu za kitaifa zinaonesha wazi nafasi muhimu ya vijana katika ustawi wa uchumi na maendeleo ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Waziri Nanauka, Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa takribani asilimia 77.3 ya Watanzania wote wana umri wa chini ya miaka 35, huku vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 35 wakichangia asilimia 34.4 ya idadi ya watu wote nchini.

Aidha, alinukuu matokeo ya Utafiti wa Nguvu Kazi ya Taifa, akisema kuwa vijana ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa uzalishaji na shughuli za kiuchumi kwa kuchangia asilimia 55.6 ya nguvu kazi ya Taifa.

“Vijana ni rasilimali muhimu sana kwa Taifa letu. Takwimu zinaonesha wazi kuwa bila kuwawezesha vijana, maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana,” alisema Nanauka.

Katika hotuba yake, Waziri huyo alisisitiza umuhimu wa majukwaa ya vijana kama hilo lililozinduliwa, akibainisha kuwa yatawasaidia vijana kupata fursa za kiuchumi, elimu ya ujasiriamali, ajira, pamoja na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao.

Uzinduzi wa jukwaa hilo unalenga kuwakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo, na kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili katika nyanja za ajira, biashara na ubunifu.

Post a Comment

0 Comments