Na. Sheila Ahmadi
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Katika kumarisha huduma za Afya nchini Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt samia imeongeza vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 8,549 Mwaka 2021 hadi vituo 9,610 Machi 2024 pamoja na maboresho ya miundombinu ya hospitali mpya katika Mikoa Mitano yaliyogharimu jumla ya Tsh: Trilioni 1.02.
Aidha Waziri. Ummy amesema kuwa Serikali imenunua vifaa Tiba vya Uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vyenye thamani ya shilingi Bilioni 290.9 ambavyo vinapatikana katika Hospitali ya Taifa,Hospitali za Rufaa, Mikoa (RRHs) na Halmashauri.
“Katika kuimarisha upatikanaji wa dawa na bidhaa za Afya, Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa na bidhaa za afya ambapo, katika kipindi cha miaka mitatu, wastani wa Shilingi Bilioni 20 zimekuwa zikitolewa kila mwezi."
" Upatikanaji wa fedha hizo umewezesha kuimarika kwa upatikanaji wa dawa muhimu na bidhaa nyingine za afya (aina 290) katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma kufikia asilimia 84% mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 58% mwaka 2022.” Amesema Ummy.
Sambamba na hayo ameongeza kuwa Miongoni mwa vifaa tiba vilivyonunuliwa ndani ya miaka Mitatu ya Rais Samia ni pamoja na MRI sita (6) jumla zimekuwa 13, Ct-Scan 32 jumla 45, Mini Angio Suit moja (1) jumla 5, Fluoroscopy moja (1) jumla 10, Digital X-ray 199 jumla 346, Ultrasound 192 jumla 668, Echocardiagram saba 7 jumla 102, Pet Scan moja ambayo haikuwepo awali pamoja na Cathlab 3 jumla zimekuwa 4
"Miaka mitatu ya Rais Samia imewezesha kuanzishwa kwa majengo mahususi ya huduma za dharura na ajali (EMDs) 105 kutoka EMD 7 zilizokuwepo mwaka 2020 ambapo majengo ya huduma za Dharura (EMD) yameongezeka na kufikia 23 katika hospitali Maalum, kanda na Mikoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba, kwa upande wa ngazi ya msingi, ujenzi wa EMD 82 katika ngazi za Halmashauri unaendelea, ambapo EMD 66 zimekamilika na zinatoa huduma na nyingine 16 ziko kwenye hatua ya ukamilishaji.”
Pia Waziri Ummy amesema ndani ya miaka Mitatu ya Rais Samia imeimarisha upatikanajo wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ikiwemo huduma za Upasuaji mgumu wa moyo bila kufungua kifua, Upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo, upandikizaji Figo, Upandikizaji Uloto, Upandikizaji wa Vifaa vya Usikivu kwa watoto, kuweka puto tumboni na upasuaji mgumu wa mifupa na mishipa ya fahamu.
Kadhalika Serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan imeimarisha huduma za Afya ya Uzazi, mama na mtoto ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Machi 2024, imekamilisha ujenzi wa jengo la kutoa huduma za afya ya Mama na Mtoto Meta iliyopo katika Jiji la Mbeya ambayo tayari inatumika na imegharimu shilingi bilioni 13.2.
Hata hivyo waziri ummy amesema Serikali ya Awamu ya sita imeendelea kufanya uwekezaji katika eneo la rasilimali watu katika afya ikiwemo kuajiri watumishi wapya wa Sekta ya Afya na kusomesha wataalamu wa afya katika fani mbalimbali za ubingwa na ubobezi ambapo hadi sasa, jumla ya wataalam 1,211 wamepata mafunzo mbalimbali ya kibingwa na bobezi na hivyo kuongeza idadi ya wataalam wa mafunzo ya kibingwa na bobezi kutoka 535 mwaka 2021 hadi 1,211 hadi kufikia sasa
0 Comments