RAIS SAMIA KUZINDUA MRADI WA BANDARI KAVU YA KWALA KIBAHA PWANI



Na Victor Masangu ,Pwani

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara mkoani Pwani Julai 31,2025 hususani katika Kata ya Kwala Halmashauri ya Kibaha Vijijini ambapo pamoja na mambo mengine Rais Samia atazindua Kongani ya viwanda ya Kwala yenye viwanda 250.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ametoa kauli hiyo Julai 22 ,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika mkutano uliofanyika katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani lililopo Manispaa ya Kibaha.

Kunenge amesema kuwa,Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan atafanya ziara katika eneo la Kwala sehemu ambayo Serikali imefanya uwekezaji mkubwa ambapo akiwa katika eneo hilo atafanya mambo mbalimbali makubwa.

Amesema Rais akiwa katika eneo la Kwala miongoni mwa shughuli atakazozifanya ni pamoja na  kuzindua safari rasmi ya treni ya Mwendokasi (SGR) ya kubeba Makasha na kupeleka Dodoma.

Ameongeza kuwa ,shughuli nyingine atakayoifanya Rais ni kuzindua bandari Kavu ya Kwala yenye uwezo wa kuhudumia Makasha 823 kwa siku na Makasha 30,000 kwa mwaka.

Kunenge amesema bandari Kavu ya Kwala itaongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam ambapo kimsingi bandari Kavu hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa Makasha katika bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 30.

Aidha ,Rais Dkt.Samia akiwa katika eneo hilo la Kwala pia atazindua maeneo ya ujenzi wa bandari Kavu kwa ajili ya nchi za Kongo, Zambia,Burundi,Malawi, Zimbabwe na Uganda ambapo pia alisema Sudan na Somalia nao tayari wameonyesha nia ya kujenga bandari Kavu katika eneo hilo.

Amesema siku hiyo itakuwa fursa kwa Rais Samia kupokea Mabehewa 160 ya Reli ya Kati ambapo kati ya hayo Mabehewa 20 yamekarabatiwa na Mabehewa 100 yamenunuliwa mapya na Serikali na mengine 40 yamekarabatiwa na Shirika la Chakula Duniani pamoja na Wakala wa Ushoroba wa Kati.

Kunenge amesema pamoja na mambo mengine lakini pia Rais Samia ataweka jiwe la msingi kwenye Kongani ya Viwanda ya Kwala yenye viwanda 250 Kongani ambayo ni kubwa katika nchi ya Tanzania.


Post a Comment

0 Comments