_Mradi wa TCCIA kwa ushirikiano na AGRA unalenga kukuza biashara za mpakani na kuimarisha usalama wa shughuli za kiuchumi_

 







 Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Mhe. Hamisi Mayamba Maiga, alizindua rasmi mahema maalumu ya kuboresha mazingira ya biashara kwa vijana na wanawake katika mpaka wa Mutukula, mkoa wa Kagera. Mradi huo, unaotekelezwa na Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture (TCCIA) kwa ushirikiano na Alliance for Green Revolution in Africa (AGRA), unahusisha ujenzi wa miundombinu ya kibiashara na mafunzo kwa wafanyabiashara wadogo.


Katika hafla hiyo, Mhe. Maiga alipongeza juhudi za TCCIA na AGRA, akisema: “Kwanza nitoe pongezi sana kwa TCCIA na AGRA kwa kuandaa mradi huu na kuutekeleza kwa viwango. Hii ni fursa kubwa kwa vijana wetu, hasa hawa wa mpakani.” Aliongeza kuwa serikali inaunga mkono jitihada hizo na kuwataka vijana kutumia mahema hayo kama jukwaa la kupata taarifa za masoko, kuripoti changamoto zisizo za kikodi, na kuongeza ufanisi wa biashara zao.


Uzinduzi uliambatana na mafunzo ya _whistle‑blowing_ kwa wafanyabiashara wa Mutukula, yaliyolenga kupambana na vizuizi visivyo vya kikodi (NTBs), kuripoti changamoto kwa njia za kidigitali, kuboresha ubora wa bidhaa, na kutumia mitandao ya kijamii kupanua masoko.


Katibu Mtendaji wa TCCIA Kagera, Bw. Rwechungura Mali, alisema chemba hiyo itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kupitia mafunzo na kuwaunganisha na mitandao ya kibiashara. “Jiunge na TCCIA ili kufungua fursa zaidi za ukuaji,” alihimiza.


Mradi, ambao tayari umeanza kutoa matokeo chanya katika mikoa ya Kigoma na Kagera, unatarajiwa kuongeza ufanisi wa biashara mpakani, kuimarisha usalama wa bidhaa, kupunguza rushwa na gharama za uendeshaji, pamoja na kukuza uchumi wa vijana na wanawake.

Post a Comment

0 Comments