Dar es Salaam, Aprili 09, 2026 – Serikali imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha sekta ya fedha nchini ili iwe chachu ya maendeleo ya haraka ya kiuchumi, huku ikisisitiza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wote kwa urahisi na gharama nafuu.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, wakati akifungua Jukwaa la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2026 jijini Dar es Salaam, lenye kauli mbiu isemayo “Sekta ya fedha bunifu na yenye uwajibikaji kwa maendeleo endelevu na jumuishi ya kijamii na kiuchumi.”
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Omar aliwataka wadau wa sekta ya fedha kutumia jukwaa hilo kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sera, sheria na mifumo ya kifedha, ili kuifikisha Tanzania kwenye uchumi imara unaotegemea sekta ya fedha ifikapo mwaka 2050.
“Mada za mwaka huu zina malengo mahsusi, na tupo katikati ya safari ya utekelezaji wa mpango wetu. Aidha, jukwaa hili pia litakuwa sehemu ya kuwasilisha dira ya maendeleo ya mwaka 2050,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali inalenga kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia sekta ya fedha, ikiwa ni pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha.
“Matumaini yetu ni kuleta mageuzi makubwa ya maendeleo na kuelekea uchumi wa dola trilioni moja za Marekani ifikapo 2050,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ali Munde, alisisitiza umuhimu wa kudhibiti hatari za kifedha, ikiwemo biashara haramu na matumizi mabaya ya mifumo ya fedha, huku akihimiza usimamizi madhubuti wa teknolojia mpya za kifedha.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Natu El Maamry Mwamba, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, sekta ya fedha imepiga hatua kubwa, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za kifedha, ongezeko la matawi na mawakala wa benki, pamoja na ukuaji wa huduma za fedha kidijitali.
Alibainisha kuwa takribani asilimia 76 ya Watanzania sasa wanapata huduma rasmi za kifedha, mafanikio yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya simu za mkononi na mifumo ya kifedha ya mtandao.
Kwa ujumla, jukwaa hilo linaonekana kuwa fursa muhimu ya kujadili mwelekeo wa sekta ya fedha nchini, huku likilenga kuimarisha mchango wake katika kukuza uchumi jumuishi na endelevu.









0 Comments