Dar es Salaam, Aprili 14, 2026 – CRDB Bank imeendelea kuwafurahisha wateja wake kwa kutoa zawadi mbalimbali kupitia promosheni yake maalum ya matumizi ya TemboCard Visa, ikiwemo tiketi za kusafiri kwenda Marekani kushuhudia fainali za Kombe la Dunia 2026.
Zawadi hizo zimetolewa katika hafla iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo yaliyopo Upanga jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kisasa.
Kupitia kampeni hiyo, wateja wanahimizwa kutumia TemboCard Visa katika malipo yao ya kila siku, iwe ni kupitia mashine za POS au kwa njia ya mtandaoni, huku kila muamala ukiongeza nafasi ya kushiriki kwenye droo mbalimbali za ushindi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Kadi (Card), Karington Chahe, alisema kampeni hiyo inalenga kuwapa wateja fursa ya kipekee ya kushinda zawadi kubwa huku wakifurahia huduma salama na rahisi za kifedha.
Alibainisha kuwa tayari droo ya kwanza imefanyika na kutoa washindi mbalimbali, huku zawadi zikiwemo runinga janja (Smart TV) zenye ukubwa wa inchi 80 pamoja na vifurushi vya DSTV kwa washindi watatu.
Aidha, zawadi kubwa zaidi katika kampeni hiyo ni tiketi nne kwa Watanzania kusafiri kwenda Marekani kushuhudia mashindano ya Kombe la Dunia 2026, yatakayowakutanisha mastaa wa soka duniani akiwemo Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
“Tunawahimiza wateja wetu kuendelea kutumia kadi zao katika malipo ya kila siku ili kuongeza nafasi ya kushinda zawadi hizi adhimu, ikiwemo safari ya kwenda kushuhudia Kombe la Dunia,” alisema Chahe.
Kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi Machi 12, 2026, ikiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya malipo ya kidijitali pamoja na kuwazawadia wateja kwa uaminifu wao kwa benki hiyo.
CRDB Bank imeeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wake wa kuendeleza ubunifu katika huduma za kifedha, huku ikiwahamasisha Watanzania kuacha matumizi ya fedha taslimu na kuhamia katika mifumo ya malipo ya kisasa iliyo salama na yenye ufanisi.
Kwa ujumla, kampeni hiyo imepokelewa kwa hamasa kubwa na wateja, huku ikitoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kushinda zawadi mbalimbali na kushiriki katika tukio kubwa la kimataifa la michezo.



0 Comments