Kinondoni, Aprili 21, 2024 – Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Warda Obathany, amewapongeza Watendaji wa Kata zote 20 za Manispaa ya Kinondoni kwa jitihada zao katika kuboresha hali ya lishe kwenye shule za msingi na sekondari ndani ya wilaya hiyo.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025 (kuanzia Januari hadi Machi), kilichofanyika katika Ukumbi wa Afya wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Warda alisema uhamasishaji wa ulaji bora na matumizi ya nishati safi umeleta mafanikio makubwa kwa wanafunzi.
“Binafsi nawashukuru na kuwapongeza Watendaji wote kwa kujitoa kwa dhati kuhamasisha ulaji unaofaa katika shule zote za Kinondoni, sambamba na matumizi ya nishati safi. Hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya lishe kwa wanafunzi wetu,” alisema Bi. Warda.
Aidha, aliwataka Watendaji hao kuendeleza juhudi hizo kwa kutoa elimu endelevu kuhusu lishe bora kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, ili kuimarisha afya na ustawi wa wananchi.
“Ni muhimu kuendeleza elimu ya lishe bora si tu mashuleni bali hadi katika ngazi ya kaya. Matumizi ya nishati safi pia yahimizwe zaidi ili kusaidia mazingira na afya,” aliongeza.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Watendaji kutoka Kata zote 20, wawakilishi wa idara mbalimbali, pamoja na wataalamu wa lishe kutoka Manispaa ya Kinondoni.









0 Comments