AIRTEL TANZANIA YAKABIDHI SERIKALI GAWIO LA SH BILIONI 65.48, YAFIKISHA SH BILIONI 350 TANGU 2019


Kampuni ya Airtel Tanzania imekabidhi Serikali gawio la Sh bilioni 65.48 kwa mwaka wa fedha 2025/26, na kufanya jumla ya gawio ililolipa Serikali tangu mwaka 2019 kufikia Sh bilioni 350. Gawio hilo lilikabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam Juni 30, 2026.

Malipo hayo yanatokana na umiliki wa Serikali wa asilimia 49 katika Airtel Tanzania PLC, na yanaifanya Airtel kuendelea kuwa kampuni pekee binafsi ya mawasiliano nchini inayolipa gawio kwa Serikali mfululizo tangu mwaka 2019. Hatua hiyo inaonyesha mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na mchango wa kampuni katika kukuza uchumi na maendeleo ya sekta ya kidijitali.

Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania PLC, Eliud Sanga, alisema gawio hilo limetokana na uwekezaji endelevu, usimamizi madhubuti wa biashara na kuzingatia misingi ya utawala bora. Alisema mbali na kutoa gawio, kampuni imeendelea kuwekeza katika huduma za mawasiliano zinazowawezesha Watanzania kufanya biashara, kupata taarifa, kujifunza na kuwasiliana kwa urahisi kupitia teknolojia.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema gawio hilo linaakisi mafanikio ya kifedha ya kampuni pamoja na imani ambayo mamilioni ya Watanzania wameendelea kuiweka katika huduma zake. Alibainisha kuwa kati ya mwaka 2021 na 2025, Airtel Tanzania imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 316 katika upanuzi na uboreshaji wa mtandao wa 4G, 5G, Home Broadband na miundombinu ya fibre ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya huduma za mawasiliano nchini.

Kamoto aliongeza kuwa kupitia Airtel Money, kampuni inaendelea kuwawezesha mamilioni ya Watanzania kupata huduma mbalimbali za kifedha kwa njia ya simu za mkononi, ikiwemo kutuma na kupokea fedha, kufanya malipo, kuweka akiba na kupata bima. Alisisitiza kuwa Airtel Tanzania itaendelea kuwekeza katika teknolojia na ubunifu ili kuunga mkono ajenda ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali na kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Post a Comment

0 Comments