William Ruto ni miongoni mwa wanasiasa wengi wakubwa nchini Kenya walioweka wazi nia zao za kuingia Ikulu ya Kenya, kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, kurithi mikoba ya aliyekuwa 'swahiba wake', Uhuru Kenyatta na nia yake sasa imetimia kwa Kishindo.
Ruto anatoka katika familia ya kawaida tu na kuwa mwanasiasa tajika nchini Kenya. Anatokea kwenye jamii ya Wakalenjin akizaliwa Disemba 21, 1966 katika kijiji cha Sugoi, magharibi mwa Rift Valley.
Elimu yake ya msingi na sekondari amesomea katika shule za kawaida kabla ya kujiunga na Chuo kikuu cha Nairobi. Waliosoma naye hasa shule ya sekondari wanamkumbuka Ruto kama 'mtu mtaratibu, mwenye haya na wakati wote akijiweka kama mtu wa kawaida tu".
“Niliuza kuku katika maeneo ambayo reli inakatiza karibu na nyumbani kwetu, nikamjengea baba yangu nyumba kwa kutumia mkopo wangu wa chuo, nikawalipia ada ndugu zangu. Mungu amekuwa mwema kwenye juhudi zangu, nashukuru nimejaliwa,” aliiambia gazeti la The Star nchini Kenya.
Kwa mujibu wa mama yake, Sara Cheruiyot, "hakuwa mkaidi" na wakati wote alikuwa 'mtiifu, mwaminifu na anayefika kwa wakati'. Hakuwa mtu anayependa ugomvi ama kugombana na wenzake, muda mwingi alikuwa akibeba kitabu kwa ajili ya kujisomea.
Akiwa chuo Kikuu, alikuwa kiongozi wa kwaya ya umoja wa wakristo chuoni hapo. Akiwa kwenye masuala hayo ya kwaya ya kanisa, alikutana na mtu aliyemuhusudu sana kwenye siasa, rais wa zamani wa nchi hiyo, Daniel arap Moi. Kama ilivyo kwa Ruto, Rais Moi pia anatokea kenye jamii ya Wakalenjini na muumini wa kanisa.
Ruto alisaidia kuanzishwa kwa kikundi cha vijana kilichoitwa Youth for Kanu 92 (YK92), ambacho Moi alikitumia kurejea madarakani mwaka 1992. Moja ya kampeni kubwa ya kikundi hicho ilikuwa ni kumwaga mabilioni ya pesa, hatua ambayo baadae ilikuja kulaumiwa kuwa chanzo cha mtikitiso wa uchumi katika miaka ya mwanzoni mwa 1990s. Inaeleweka kwamba wakati huu, ndio Ruto alipotengeneza utajiri wake.

0 Comments