SERIKALI YATENGA BILIONI 28 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), imetenga Shilingi bilioni 28 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara nchini.


Akizungumza katika semina iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Ismaily Mafita, alisema kuwa mafunzo hayo yalilenga kuwapa wanahabari wa mitandao ya kijamii elimu juu ya ujenzi wa madaraja na barabara, ili waweze kuelimisha umma kwa usahihi.


"Kupitia semina hii, tunatarajia kuwa wananchi wataelewa umuhimu wa kuhifadhi barabara, kwani zinatumika kwa zaidi ya asilimia 80 ya usafirishaji wa bidhaa na watu," alisema Mhandisi Mafita.


Aliongeza kuwa TARURA imejenga zaidi ya kilomita 5,000 za barabara katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam. Aidha, wakala huo unatumia teknolojia mbadala kama ujenzi wa madaraja ya mawe, jambo linalosaidia pia kuongeza ajira kwa vijana wasio na ujuzi wa kiufundi.


Mhandisi Mafita alibainisha kuwa baadhi ya miradi ya miundombinu inaendelea kutekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia awamu ya pili ya Mradi wa DMDP. Mradi huu unahusisha ujenzi wa barabara na mifereji ya mvua jijini Dar es Salaam.


Kwa upande wake, Dkt. Heladius Makene kutoka Kitengo cha Mazingira na Jamii alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kuboresha barabara za mijini na vijijini kupitia TARURA.


Naye Mhandisi Pharles Ngeleja alieleza kuwa mwaka 2024, jumla ya kilomita 3,000 za barabara zimejengwa nchini, huku serikali ikiendelea kuwekeza katika barabara za lami na zege mijini na vijijini. Aliongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaathiri miundombinu, hivyo TARURA inatumia vifaa vinavyopatikana kwenye maeneo husika ili kuhakikisha ujenzi unakuwa wa kudumu.


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Humphrey Shayo, aliipongeza TARURA kwa kutambua mchango wa wanahabari wa mitandao ya kijamii katika kusambaza taarifa kwa haraka na kuwahabarisha wananchi kuhusu maendeleo ya miundombinu.






Post a Comment

0 Comments