Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amewataka wahitimu wa Taasisi ya UONGOZI kuwa viongozi waadilifu, wabunifu na wenye uthubutu ili kuchochea maendeleo endelevu ya taifa.
Akizungumza Mei 15, 2026 katika mahafali ya tisa ya UONGOZI Institute yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Kikwete amesema uongozi si cheo bali ni dhamana ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Amesema wahitimu hao wanawakilisha nguvu mpya ya uongozi barani Afrika, akieleza kuwa kupitia mafunzo waliyopata wamejengewa uwezo wa kusimamia nafsi, watu na taasisi kwa ufanisi zaidi.
“Uongozi bora unahitaji uadilifu. Katika ulimwengu wa leo, kiongozi bora hupimwa kwa uwezo wake wa kusimamia haki, uwazi na matumizi sahihi ya rasilimali za umma,” amesema.
Aidha, amewahimiza wahitimu kutumia maarifa waliyopata kubuni suluhisho za changamoto za kijamii na kiuchumi, huku akisisitiza kuwa hawapaswi kuridhika na vyeti walivyopata bali waendelee kujifunza na kutafuta fursa mpya.
Katika hotuba yake, Kikwete pia ameipongeza Taasisi ya UONGOZI kwa kutimiza miaka 15 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2010, akieleza kuwa imekuwa na mchango mkubwa katika kuandaa viongozi wenye uwezo na weledi barani Afrika.
Ametoa shukrani kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Serikali ya Finland, Umoja wa Ulaya pamoja na taasisi za kimataifa kwa kuendelea kuisaidia taasisi hiyo kufikia malengo yake.
Kwa upande mwingine, amewakumbusha wahitimu kuwa kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kunahitaji uwepo wa viongozi bora wenye maono, akibainisha kuwa mipango mizuri haiwezi kufanikiwa bila uongozi thabiti.
“Tunataka Tanzania yenye uchumi imara, shirikishi na shindani. Hata hivyo, dira hiyo haiwezi kufikiwa bila kuwa na viongozi waadilifu wanaolinda mali za umma na kusimamia maendeleo ya wananchi,” amesisitiza.
Amehitimisha kwa kuwataka wahitimu kwenda kuwa chachu ya mabadiliko katika maeneo yao ya kazi na jamii, huku akitangaza rasmi kufunguliwa kwa mahafali hayo.
Mwisho wa hafla hiyo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Yahaya Nawanda, Mbunge wa Newala; Juma Mkomi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Neema Jamu, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Ikulu; Dkt. Elsie Sia Kanza, Balozi wa Tanzania nchini Marekani; Ombeni Sefue, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI; pamoja na Kadari Singo, Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo.
Aidha, mahafali hayo yalihusisha wahitimu wa programu mbalimbali za uongozi zikiwemo Stashahada ya Uzamili ya Uongozi (Postgraduate Diploma in Leadership), Programu ya Uongozi Ngazi ya Cheti (Certificate in Leadership), Programu ya Uongozi kwa Wanawake (Women’s Leadership Programme) pamoja na Programu ya Uongozi kwa Viongozi Chipukizi (Emerging Leaders Programme).



0 Comments