Benki ya CRDB Bank imeendelea kuwazawadia wateja wake kupitia kampeni ya matumizi ya Tembo Card, ambapo washindi mbalimbali wamejinyakulia TV za nchi 85 pamoja na nafasi ya kwenda kushuhudia mashindano ya Kombe la Dunia mwaka huu nchini Canada.
Akizungumza katika zoezi la kutangaza washindi wa kampeni hiyo, viongozi wa benki hiyo wamesema mwezi uliopita tayari walipatikana washindi wanne wa safari ya kwenda Marekani pamoja na washindi watatu wa TV, huku leo wakitarajia kuendesha droo nyingine ya kupata washindi sita zaidi.
Aidha, CRDB imewahamasisha Watanzania kuendelea kutumia Tembo Card pamoja na huduma za malipo ya kidigitali ili kuongeza nafasi za kushinda zawadi mbalimbali zinazotolewa kupitia kampeni hiyo.
“Tumia Tembo Card yako ili uweze kuwa mshindi kwa sababu ushindi bado unaendelea. Hakuna benki yoyote inayowapeleka washindi kwenda kuangalia Kombe la Dunia isipokuwa CRDB,” ilielezwa katika hafla hiyo.
Vilevile, benki hiyo imewataka wananchi ambao bado hawajawa wateja wa CRDB kufika katika matawi mbalimbali ya benki hiyo ili kupata Tembo Card zao kwa haraka.
“Kwa sasa mteja anafika tawi lolote la CRDB na anapata card yake hapo hapo, tofauti na zamani ambapo wengine walikuwa wakisubiri kwa siku kadhaa,” ilielezwa.
Katika droo hiyo, washindi watatu wamejishindia TV za nchi 85 ambao ni pamoja na Amina Kaswala Awadhi, mkazi wa Kijichi, pamoja na Esther Dawson Kabakama na Lusekelo Michael.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Amina amesema mara nyingi amekuwa akitumia kadi kulipia bidhaa mbalimbali bila kujua kuwa alikuwa akishiriki kwenye droo ya ushindi.
“Mara nyingi nikikuwa nanunua vitu natumia card kulipia, sikuwa na idea kwamba ninavyo lipia nipo kwenye droo ya kushinda. Nimefurahi sana,” amesema.
Kwa upande mwingine, washindi wa safari ya kwenda Canada kushuhudia mashindano ya FIFA World Cup ni pamoja na Abdulrauf Suleiman Muta, mkazi wa Upanga, Charles Makongoro Nyerere, pamoja na Arun Vithaldas Lodhia.
Akizungumza baada ya kushinda, Charles Makongoro amesema aliifahamu CRDB tangu kipindi benki hiyo ilipofungua huduma vijijini.
“Kwa mara ya kwanza niliwafahamu nilipokuwa kijijini baada ya CRDB kufungua tawi. Zamani matumizi ya card hayakuwa makubwa lakini sasa watu wengi wanafurahia na kutumia CRDB Kiganjani,” amesema.
CRDB imeendelea kusisitiza kuwa kampeni hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kidigitali pamoja na kuwapa motisha wateja kutumia Tembo Card katika miamala yao ya kila siku.

0 Comments