Salum Mwalimu na Devotha Minja kupeperusha bendera ya Chaumma kwenye mbio za urais Tanzania

 





Katibu Mkuu wa chama cha Ukombozi wa Umma, Chaumma, Salum Mwalimu atakuwa mpeperusha bendera wa chama hicho kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Tanzania mwezi Oktoba mwaka huu.


Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Benson Kigaila amemtangaza Mwalimu katika mkutano mkuu wa chama hicho hii leo


Kigaila amesema jina hilo lilipendekezwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho yenye jukumu la kuleta jina la mgombea urais Tanzania na Zanzibar, katika kikao kilichofanyika jana Jumatano.


Mwalimu alihamia Chaumma akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kuondolewa katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar mapema mwaka huu.


Katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020, Salum Mwalimu alikuwa mgombea mwenza wa urais kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati mgombea urais alikuwa Tundu Lissu aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 13 nukta sifuri nne ya kura nyuma ya mshindi John Magufuli wa CCM aliyepata asilimia 84 nukta nne.


Salum Mwalimu ni mwandishi wa Habari kitaaluma, aliwahi kufanya kazi katika vituo kadhaa vya radio nchini Tanzania. Pia aliwahi kufanya kufanya kazi katika kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom kabla ya kuingia katika siasa.


Uteuzi wa Chauma umekuja siku moja baada ya chama cha ACT-Wazalendo kumtangaza Waziri wa zamani mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina kuwa mgombea wake wa urais. Chama tawala kilikwishakumteua mgombea wake, Samia Suluhu Hassan katika mkutaano mkuu uliofanyika jijini Dodoma Januari mwaka huu.


Wote hao na wengine-iwapo watakuwepo-watangoja kuthibitishwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) baadaye mwezi huu Agosti, kuwa wagombea rasmi kupitia vyama vyao.

Post a Comment

0 Comments