Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Hafla ya utoaji wa Tuzo za Best Brand Africa kwa mwaka 2025 imefanyika kwa mafanikio makubwa katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Septemba 21, ikishirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi. Tuzo hizi zilitolewa kwa lengo la kutambua na kuenzi kampuni na taasisi bora ambazo zimejipambanua katika ujenzi wa chapa imara, ubunifu wa huduma, na mchango chanya kwa jamii.
Muandaaji wa tuzo hizo, Ndg. Zakayo Shushu, alisema kuwa hafla hiyo ni mwanzo wa mchakato mkubwa wa kutangaza ubora wa chapa za Kiafrika ndani na nje ya bara. Alieleza kuwa pamoja na tuzo kuanza hapa nchini, malengo makubwa ni kuzifikisha hadi ngazi ya Afrika nzima.
> "Tumeanza hapa Tanzania, lakini dhamira yetu ni kuzifikisha tuzo hizi katika kila pembe ya Afrika. Mwaka ujao tumejipanga vizuri zaidi," alisema Zakayo Shushu mbele ya wageni waalikwa.
Tuzo za Best Brand Africa zimeanzishwa kwa malengo maalum ya kuonyesha hadhi ya chapa bora barani Afrika, ambazo zimefanya vizuri katika utoaji wa huduma bora, bidhaa zenye viwango, pamoja na uaminifu kwa wateja wao. Kupitia tuzo hizi, kampuni hupata nafasi ya kutambulika, pamoja na kuhimizwa kuendelea kuwekeza katika ubunifu, uboreshaji wa huduma na mikakati ya kuimarisha chapa zao.
Katika hotuba yake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Dkt. Kedmon E. Mapana, alionesha kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na Zakayo Shushu katika kukuza sekta ya chapa kupitia tuzo hizi. Alimtambua Zakayo kama kijana mwenye maono ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kusaidia kukuza vipaji na taasisi za kijamii na kiuchumi.
> "Zakayo amefanya kazi nzuri. Tunamtambua hata alipokuwa anamsaidia Madam Ritha kwenye kipindi cha BSS. Hizi brand names ni muhimu na tunapaswa kuzilinda. COSOTA ipo, na haya yote ni sehemu ya kupeana moyo na kuonyesha kwamba tunaweza kufanya mambo kwa tofauti," alisema Dkt. Mapana.
Tukio hilo lilihusisha utoaji wa tuzo kwa makampuni mbalimbali, pamoja na watu binafsi waliotambuliwa kwa mafanikio yao katika nyanja tofauti kama biashara, sanaa, serikali na huduma kwa jamii. Washindi walipokea tuzo zao kwa furaha kubwa, huku wakiahidi kuendelea kutoa huduma bora na kuwa mabalozi wa chapa zao.
Zakayo Shushu alimalizia kwa kusema kuwa mwaka ujao tuzo hizo zitakuwa kubwa zaidi kwa kushirikisha mataifa mengi ya Afrika, huku akitoa wito kwa makampuni yote kuzingatia ubunifu na ubora kama nguzo ya ujenzi wa chapa.
> "Best Brand Africa sio tu tuzo, bali ni harakati ya kuonyesha kuwa Afrika inaweza kujenga chapa imara zinazotambulika duniani," alisisitiza.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa tafrija fupi ya kuwapongeza washindi, huku wageni waalikwa wakipata fursa ya kuunganishwa kibiashara na kijamii kupitia mazungumzo ya kando (networking



0 Comments