ASILIMIA 39.5 YA WANAWAKE WAATHIRIKA WA UKATILI, SERIKALI YATAHADHARISHA UKATILI WA KIDIJITALI



Serikali imesema ukatili wa kijinsia unaendelea kuwa changamoto kubwa ya haki za binadamu nchini, huku takwimu zikionesha kuwa asilimia 39.5 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamewahi kukumbwa na ukatili wa aina mbalimbali, ikiwemo wa kimwili, kihisia na kingono.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kitaifa kuhusu ukatili wa kijinsia unaofanyika kupitia teknolojia (TFGBV), Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Abeda Rashid Abdallah, alisema tatizo hilo linaongezeka kwa kasi na linahitaji hatua za haraka.

Mkutano huo uliandaliwa na United Nations Population Fund kwa kushirikiana na C-Sema, ukiwa na lengo la kuimarisha juhudi za kukabiliana na ongezeko la ukatili wa kidijitali dhidi ya wanawake na wasichana.

Abeda alifafanua kuwa ukatili wa kidijitali unajumuisha vitendo kama usambazaji wa picha za faragha bila ridhaa, unyanyasaji wa kingono mtandaoni, vitisho pamoja na lugha za chuki, hali inayowaathiri kwa kiasi kikubwa kisaikolojia na kijamii waathirika wake.

Alibainisha kuwa zaidi ya nusu ya wanawake vijana wamewahi kukumbana na unyanyasaji mtandaoni, jambo linaloongeza hofu katika kipindi hiki cha kukua kwa matumizi ya teknolojia.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa United Nations Population Fund nchini, Melissa Barrett, alisema teknolojia inapaswa kuwa chombo cha uwezeshaji badala ya kuwa jukwaa la madhara.

“Ni muhimu ubunifu wa kidijitali uchangie katika kukuza usawa wa kijinsia na kulinda haki za binadamu,” alisema.

Naye Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting, alisema ushirikiano kati ya serikali yake, UNFPA na Tanzania unalenga kuboresha usalama wa mtandao na matumizi salama ya teknolojia.

Aidha, Ofisa Programu za Jinsia kutoka United Nations Population Fund, Ally Ahmad, alisema mkutano huo ni muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja na kuandaa mikakati madhubuti ya kukabiliana na ukatili huo.

Wadau wameitaka jamii kuimarisha usalama wa kidijitali na kuchukua hatua madhubuti ili kulinda wanawake na wasichana, na kuhakikisha wanapata nafasi salama ya kushiriki katika elimu, uchumi na maisha ya kijamii.

Post a Comment

0 Comments