Julieth Kabyemela, Mkurugenzi Msaidizi wa Urithi wa Utamaduni na Maendeleo ya Taifa na Kaimu Mkurugenzi kutoka Wizara ya Habari, amesema Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika kupitia mafunzo ya kijeshi na msaada wa kidiplomasia kwa vyama mbalimbali vya ukombozi.
Akizungumza katika maadhimisho ya SADC Day yaliyofanyika leo Machi 23, 2026 katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Dkt. Kabyemela alisema siku hiyo ni muhimu katika kukumbuka ushindi wa ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.
Alieleza kuwa maadhimisho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Southern African Development Community, ambapo mataifa mbalimbali ya Afrika yanaungana kufanya kumbukizi hiyo kupitia shughuli tofauti zinazolenga kuenzi historia ya ukombozi.
Dkt. Kabyemela alisisitiza kuwa pamoja na mafanikio ya kisiasa, bado kuna haja ya kuendeleza mapinduzi ya kiuchumi ili kuimarisha uhuru wa kweli wa bara la Afrika.
Aidha, alitoa wito kwa vijana kuwa walinzi wa urithi huo, wakihakikisha simulizi za ukombozi hazipotei bali zinatumika kujenga uzalendo na dira ya Afrika inayotakiwa.
“Ni jukumu letu kuhakikisha historia hii inaenziwa na kujifunza kutoka kwa waasisi wetu ili tuweze kusonga mbele pamoja kuelekea mapinduzi ya kiuchumi,” alisisitiza.
Alimalizia kwa kusisitiza mshikamano miongoni mwa Waafrika, akieleza kuwa urithi wa ukombozi ni tunu inayopaswa kulindwa na kuendelezwa kwa vitendo, huku akiwahimiza vijana kuwa mstari wa mbele katika kuijenga Afrika yenye kujitegemea, umoja na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.




0 Comments