DAR ES SALAAM
Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Doha (Doha Dialogue) kuhusu uhamaji wa nguvu kazi na ajira, utakaofanyika Oktoba 5 na 6, 2026 jijini Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya ajira na kufungua fursa zaidi za ajira kwa Watanzania nje ya nchi.
Mkutano huo utafanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency na unatarajiwa kuwakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 33 za Afrika, nchi za Ghuba, Jordan na Lebanon kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuendeleza uhamaji salama wa nguvu kazi pamoja na ajira zenye staha.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Mhe. Deus Sangu, amesema Tanzania ni nchi ya pili duniani kuwa mwenyeji wa Doha Dialogue na ya kwanza barani Afrika kuandaa mkutano huo muhimu.
Amesema ajenda kuu za mkutano huo zitajumuisha kujadili mikataba ya ajira baina ya nchi, ulinganifu wa ujuzi wa wafanyakazi na mahitaji ya soko la ajira, pamoja na maandalizi ya nguvu kazi kukabiliana na mabadiliko yanayoletwa na maendeleo ya teknolojia.
Kwa mujibu wa Waziri Sangu, Tanzania itatumia jukwaa hilo kueleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika soko la ajira la kimataifa, huku ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda haki za wafanyakazi na kuhakikisha upatikanaji wa ajira zenye staha.
Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo, “Kutoka Ahadi hadi Vitendo: Kuendeleza Uhamaji wa Nguvu Kazi wenye Haki na Endelevu wa Nchi za Afrika na Ghuba (GCC+).”

0 Comments