Gairo, Morogoro
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo (DED), Bi. Sharifa Nabalang’anya, amekutana na kufanya kikao kazi na wenyeviti wa vijiji, vitongoji, watendaji wa kata pamoja na wajumbe wa kamati za mazingira, kwa lengo la kujadili na kuimarisha suala la usafi katika maeneo yao.
Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Sharifa alisema lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kusikiliza maoni na changamoto kutoka kwa kila upande, ili kwa pamoja waweze kupata suluhisho la kudumu kuhusu masuala ya usafi wa mazingira katika wilaya ya Gairo.
“Tumejadiliana kwa kina na kukubaliana kushirikiana kwa karibu zaidi katika kusimamia na kuboresha usafi, kwani suala hili linahitaji mshikamano wa wadau wote,” alisema.
Aidha, wenyeviti wa vijiji na vitongoji waliwasilisha ahadi yao ya kuimarisha ushirikiano na mamlaka ya halmashauri, ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Bi. Sharifa aliwakumbusha wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba waliyoingia na halmashauri, huku akisisitiza kuwa uzembe hautavumiliwa.
Pia aliwatambulisha wananchi mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, sambamba na kuhimiza usajili wa daftari la wakazi, akibainisha kuwa mipango hiyo ni muhimu katika kuboresha huduma za kijamii na ustawi wa wananchi.
Alisisitiza kuwa jukumu la usafi si la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira.






0 Comments