MWENGE WA UHURU 2026 UMEZINDUA MRADI WA NISHATI SAFI SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA GALIJEMBE

 Na mwandishi wetu,Mbeya

Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 umezindua Mradi wa Ujenzi wa Mfumo wa Matumizi ya Nishati Safi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Galijembe, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ukiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034.

Mradi huu umegharimu jumla ya Shilingi 39,493,212/-, ambapo Shilingi 20,593,212/- zimetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira kupitia Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai Tanzania (SLR), huku Shilingi 18,900,000/- zikiwa ni mchango wa Halmashauri kupitia mapato ya ndani.

Mradi unahusisha ujenzi wa mfumo wa gesi ya LPG wenye uwezo wa kilogramu 500, ununuzi wa majiko ya gesi na majiko banifu yanayotumia kuni poa, pamoja na ukarabati wa jiko la shule. 

Aidha Utekelezaji wake umefikia asilimia 100 na tayari unatumika kwa wanafunzi takribani 522, huku elimu ya usalama na matumizi ya mfumo huo ikitolewa na Jeshi la Zimamoto na vifaa vya kuzimia moto kuwekwa katika maeneo muhimu ya shule.

Matumizi ya nishati safi yanatarajiwa kupunguza utegemezi wa kuni za miti, uchafuzi wa hewa na ukataji wa miti, sambamba na kuboresha mazingira na afya za watumiaji. 

Aidha, mradi huu umesaidia kupunguza gharama za nishati shuleni kutoka takribani Shilingi milioni 14 kwa mwaka kwa matumizi ya kuni za kawaida hadi Shilingi milioni 12 kwa matumizi ya kuni poa, huku matumizi ya gesi yakitarajiwa kupunguza zaidi gharama hizo.


Post a Comment

0 Comments