Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Daktari Samia Suluhu Hassan imedhamiria kusimamia maslahi ya Askari wa Jeshi la Polisi na ndio maana imetenga bajeti maalum ili kuboresha miundo mbinu kama vile kujengwa kwa vituo vya Polisi, nyumba za Askari, kuboresha mifumo ya utendaji ili kuendana na hali ya usasa katika ulimwengu wa Teknolojia.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango Katika ufunguzi kituo cha Polisi Daraja "A " Wilaya ya Kigamboni leo tarehe 28/04/2023 ambapo amesema kituo hicho kiwe ni chachu katika utendaji kazi utakaozingatia haki kwa jamii kwani endapo haki itakosekana maendeleo ya nchi pia hayawezi kustawi.
Amesema Askari wa Jeshi la Polisi ni kioo katika jamii, hivyo ni vyema kujenga uhusiano mzuri na wananchi kwa kushirikiana nao katika mifumo ya ulinzi shiriki sambamba na kupata taarifa mbalimbali za kihalifu na wahalifu kwa vile wananchi wao ndio wanaoijua jamii wanazoishi nazo.
Aidha amekemea vikali tabia ya baadhi ya Askari kuwabambikizia kesi wananchi, kuchelewa kwa upelelezi, kuomba rushwa hususani kwa Askari wa Usalama Barabarani na kupelekea madereva wengi kukiuka sheria za usalama barabarani na hatimae kusababisha ajali zisizo za lazima.
Akifafanua juu ya suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii Dkt Mpango amesema kuwa kila mzazi kwa nafasi yake ajitahidi kusimamia malezi bora kwa watoto, aidha ameliagiza Jeshi la Polisi kufuatilia kwa ukaribu baadhi ya Saloni ambazo zimekuwa zikifanya kazi kinyume na utaratibu wa kimaadili ili kuweza kuwachukilia hatua za kisheria watakaobainika.
Akizungumzia kuhusu utunzaji wa mazingira amesema upandaji miti ni lazima kwa wananchi wote ili kutunza mazingira ya viumbe hai, katika hatua hiyo amesema kukata mti ni uhalifu kama uhalifu mwingine.
kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya NChi Mhe. Muhandisi Hamad Masauni ameishukuru Serikali kwa bajeti iliyopitishwa yenye lengo la kuimarisha miundobinu na maslahi ya Askari wa Jeshi la Polisi.
Amesema kwamba uzindizi wa majengo mbalimbali Nchini katika maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano waTanganyika na Zanzibar yaliyoasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheik Abeid Aman Karume ambayo yanajenga udugu wa dhati na mchanganyiko juu ya pande mbili, amesema "ubunifu wa miradi mbalimbali utasaidia
vizazi vya sasa kujua chimbuko na historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar".
Mhe. Masauni amesema atahakikisha pesa iliyotolewa katika miradi inatumika kama malengo yaliyotarajiwa na endapo yeyote ataenda kinyume hatua za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Ameongezea kwa kusema kuwa Serikali inatambua mchango unaotolewa na Jeshi la Polisi Nchini kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama Nchini ndio maana walifanikiwa kudhibiti matukio mbalimbali Nchini ikiwa ni pamoja na mauji ya Albino mauaji Kibiti na Panya Road.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP. Camillus Wambura amesema kuwa Kituo cha Polisi Wilaya ya Kigamboni ni kituo chenye hadhi ya Kimataifa, na amesema uwepo wa kituo hicho unaendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao.
IGP. Camillus Wambura amewataka askari kufanya kazi kwa nidhamu, haki, weledi na uadilifu pia amewataka kutumia jengo hilo la kituo kuakisi hisia za haki kwa wale watakao kwenda kupata huduma kwenye kituo hicho na vituo vyote nchini.
Aidha katika kutambua umuhimu wa mazingira na kutunza mazingira miche 400 ya matunda na kivuli imepandwa kuzunguka eneo hilo la kituo.
Ujenzi wa Kito hicho cha Polisi unakwenda kusogeza huduma za Polisi karibu zaidi na wananchi kufuatia kukua kwa kasi kwa Wilaya hiyo ya Kigamboni.
Viongozi mbalimbali wa chama na Serikali, viongozi wa dini, Vyombo vya ulinzi na usalama, wandishi wa habari na Wananchi walihudhuria katika ufunguzi huo.








0 Comments