Na Mwandishi wetu
RAIS na Mwenyekiti wa Bodi ya Chemba ya
Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Vicent Minja ametaja malengo makuu sita (6) ambayo wanatarajia kuyafanya ndani ya siku 100 za uongozi wake.
Minja ametaja mambo hayo akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 10, 2023 jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutangaza rasmi Bodi mpya ya TCCIA iliyochaguliwa na Mkutano Mkuu uliofanyika Novemba 7 Mwaka huu.
Mambo hayo ni pamoja na kuimarisha ushirikiano, kukuza Maendeleo ya Sekta, kuendeleza ubunifu na Teknolojia katika utoaji wa vyeti vya uasili (Certificate of Origin), kukuza Umoja na mshikamano ndani ya Chemba, ushirikiano na Serikali, Taasisi, Balozi na wadau wa Maendeleo na kusimamia mabaraza ya Biashara na kuendelea kuhudumia Sekta binafsi.
Kuhusu kuimarisha ushirikiano Minja amesema Bodi mpya itaweka msisitizo katika kujenga ushirikiano wa dhati na wanachama, wafanyabiashara na wadau wote.
“Tutahakikisha kuwa sauti za wanachama zinasikika na kuzingatiwa katika kila hatua tunayochukua,” amesema Minja.
Akizungumzia kuhusu kukuza Maendeleo ya Sekta, amesema wataendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali, na wadau wengine kuhakikisha kuwa Biashara, Viwanda na Kilimo vinapiga hatua mbele.
Kwamba wataweka mikakati imara ya kuvutia uwekezaji, kutoa Mafunzo na kusaidia Miradi inayochangia ukuaji wa Sekta hizi.
Kwa upande wake Makamu wa Rais, Biashara Boniphace Ndengo amesema atahakikisha anachochea mageuzi na mapinduzi ya masoko ndani na nje ya nchi.
Kadhalika ameeleza kuwa atapambana kuweka Mazingira ya upatikanaji kwa mikopo ya mitaji ili kuwezesha kuanzishwa kwa Biashara mpya.
Kwamba atahakikisha kunakuwa na ujenzi wa Makampuni makubwa amabayo yanaweza kufanya wigo wa Biashara ndani na nje ya nchi.
Naye Makamu wa Rais, Kilimo Swallah S. Swallah amesema watahakikisha wanaimarisha Taasisi ya TCCIA ili kukuza Sekta ya Kilimo kwani zaidi ya silimia 90 ya Watanzania wapo katika Sekta ya Kilimo.
Bodi mpya ya TCCIA iliyochaguliwa hivi karibuni inaundwa na Rais na Mwenyekiti wa Bodi Vicent Ninja, Makamu wa Rais, Biashara Boniphace Ndengo, Makamu wa Rais, Viwanda Abdul Mwilima na Makamu wa Rais, Kilimo Swallah S. Swallah.

0 Comments