MKURUGENZI GAIR0 ATOA WITO KWA WATUMISHI KUWAFIKIA WANANCHI KWA HUDUMA BORA

 

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Bi. Sharifa Nabalang’anya, aliwataka watumishi na wataalamu wa ngazi ya kata na vijiji kuhakikisha wanawafikia wananchi kwa kuwahudumia kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu ili kuimarisha taswira chanya ya Serikali.


Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri Novemba 25, Bi. Nabalang’anya alisema wananchi wanahitaji kuona matokeo ya kazi zinazofanywa na Serikali kupitia huduma bora, stahiki na zinazotolewa kwa wakati, sambamba na kuimarisha ukaribu na usikivu kwa wananchi.


Alisema tabasamu la wananchi linatokana na namna watumishi wanavyotekeleza majukumu yao ya kila siku kwa uadilifu na uwajibikaji, huku akisisitiza kila mtumishi kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii.



Aidha, aliwakumbusha watendaji wa kata na vijiji kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato, usafi wa mazingira pamoja na utekelezaji wa afua mbalimbali zinazolenga kuboresha ustawi wa jamii.


Katika hatua nyingine, Bi. Nabalang’anya aliwataka watumishi hao kuongeza ubunifu katika kutatua changamoto zinazokabili jamii, hususan katika sekta za kilimo, mifugo na afya, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na ngazi za Halmashauri, hasa kwa vijana, kwa kuwaonesha fursa mbalimbali zitakazowezesha kuwakwamua kiuchumi kupitia miradi ya maendeleo.



Post a Comment

0 Comments