Dar es Salaam, Desemba 28, 2025
Chama cha Wamachinga Tanzania kwa kushirikiana na waendesha boda boda na bajaji leo kimezungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kikieleza maandalizi ya kongamano kubwa la kitaifa linalotarajiwa kufanyika mwezi Januari, 2026.
Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa viongozi wa chama hicho alisema kuwa kongamano hilo halitawahusisha wao pekee, bali litawakutanisha pia viongozi wakuu wa serikali, kwa lengo la kuwasilisha changamoto zinazowakabili wamachinga, boda boda na bajaji nchini.
“Katika kongamano hili kubwa, hatutakuwa sisi peke yetu. Tutakuwa na kiongozi mkubwa wa serikali ili kumueleza changamoto zinazowakabili boda boda na bajaji moja kwa moja,” alisema kiongozi huyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Machinga Tanzania aliwashukuru wamachinga na mama lishe kwa kuonesha uzalendo na nidhamu kwa kutoshiriki maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika tarehe 9 na 25 Desemba.
“Nawashukuru sana wamachinga na mama lishe kwa kutii wito wa amani na kutoshiriki maandamano katika tarehe hizo. Hatua hii imeonesha mshikamano na upendo wa nchi,” alisema.
Aliongeza kuwa maandalizi ya kongamano la kitaifa yanaendelea vizuri, huku akisisitiza kuwa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wadogo na waendesha vyombo vya usafiri zinahitaji ufumbuzi wa haraka katika maeneo yote ya nchi.
Akizungumzia changamoto hizo, Mwenyekiti huyo alisema kuwa changamoto ya kwanza kwa waendesha boda boda ni kukosa mikopo kwa wakati, hali inayokwamisha juhudi zao za kujiendeleza kiuchumi.
“Boda boda wengi wanakosa mikopo kwa wakati. Tunaomba taasisi za kifedha na serikali kuwafikia ili waweze kujikwamua kiuchumi,” alisisitiza.
Aidha, alieleza kuwa waendesha boda boda hukaa muda mrefu juani wakisubiri wateja, hivyo akaomba serikali itengeneze miundombinu rafiki kama maeneo ya kupumzikia na kujisitiri wakati wa kusubiri huduma.
Changamoto ya pili aliyoitaja ni fursa za kifedha, ambapo alieleza kuwa tayari Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na makundi maalum, huku akiomba fedha hizo ziwafikie walengwa kwa wakati na kwa uwazi.
Pia aligusia changamoto ya mgambo wanaodaiwa kuwasumbua wamachinga katika maeneo mbalimbali, akiiomba serikali kuwatafutia ajira rasmi ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima mitaani.
“Mgambo nao ni Watanzania wenzetu. Tunaomba watafutiwe kazi mbadala ili kuondoa migogoro na kuwapa wananchi mazingira ya kufanya kazi kwa amani,” alisema.
Kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kitaifa litakalowakutanisha wadau mbalimbali, likiwa na lengo la kusikiliza, kujadili na kutatua changamoto zinazowakabili wamachinga, boda boda na bajaji nchini.


0 Comments