WAUMINI WAWILI WAIOMBA VATICAN ICHUNGUZE MWENENDO WA PADRI KITIMA

 




Dar es Salaam

Waumini wawili wa Kanisa Katoliki nchini, Stanslaus Thobias Nyakunga na Elia Phaustine Kabote, leo Desemba 25, 2025, wameiandikia Vatican kupitia Balozi wake nchini Tanzania, Askofu Mkuu Angelo Accattino, wakiomba kufanyika kwa uchunguzi wa kichungaji na kiutawala kuhusu mwenendo wa Padri Dkt. Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).

Katika barua yao, waumini hao wamesema kuwa kwa muda mrefu kumekuwapo mitazamo ndani ya jamii inayodai kuwa Padri Kitima ameonekana kujihusisha au kuingilia masuala ya siasa, hususan migogoro ya ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hali ambayo, kwa mujibu wao, haijajitokeza kwa kiwango kama hicho kwa vyama vingine vya siasa.

Wamesema kuwa madai hayo, bila kujali kama yana ukweli au la, yameanza kuathiri taswira ya Kanisa Katoliki miongoni mwa waumini na kwa umma kwa ujumla, jambo linaloweza kulifanya Kanisa lionekane kama linachukua upande wa kisiasa, kinyume na jukumu lake la msingi la kuwa taasisi ya amani, maridhiano na mwongozo wa kimaadili katika jamii.

Nyakunga na Kabote wamesisitiza kuwa hatua yao haikulenga kutoa tuhuma wala kumshambulia Padri Kitima binafsi, bali kuomba mamlaka ya juu ya Kanisa kuingilia kati kwa hekima ya kichungaji, kufanya uchunguzi na kutoa mwongozo wa wazi utakaolinda umoja wa waumini na heshima ya Kanisa.

Katika kuunga mkono hoja zao, waumini hao wamenukuu Maandiko Matakatifu yanayowataka viongozi wa Kanisa kuwa wajenzi wa amani na mshikamano. Wamenukuu maneno ya Yesu Kristo yasemayo, “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mathayo 5:9), pamoja na kauli ya Mtume Paulo isemayo, “Mungu si wa machafuko bali wa amani” (1 Wakorintho 14:33), sambamba na onyo dhidi ya migawanyiko miongoni mwa waumini (1 Wakorintho 1:10).

Hatua hiyo imechukuliwa katika kipindi ambacho nchi inapitia mjadala mpana wa kisiasa na kijamii, hali inayoongeza matarajio kwa taasisi za dini kuendelea kubaki nguzo za utulivu, upatanisho na mshikamano wa kitaifa bila kujihusisha na mvutano wa vyama vya siasa.

Kwa mujibu wa barua hiyo, waumini hao wameiomba Holy See kushughulikia masuala matatu makuu, yakiwemo kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mwenendo wa Padri Kitima, kutoa mwelekeo wa wazi unaothibitisha uhuru wa uongozi wa Kanisa dhidi ya siasa za vyama, pamoja na kuchukua hatua zitakazolinda umoja wa waumini, amani ya jamii na mamlaka ya kimaadili ya Kanisa.

Waumini hao wameeleza imani yao kuwa Vatican ina busara, uzoefu na mamlaka ya kushughulikia suala hilo kwa maslahi mapana ya Kanisa na jamii kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments